IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema Uislamu ni dini ya masuala ya kiroho na sayansi

10:47 - March 30, 2010
Habari ID: 1900780
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei amekagua moja ya viwanda vikubwa nchini Iran na kushuhudia kwa karibu sehemu ya uwezo wa kiviwanda wa taifa hususan katika sekta ya utengenezaji magari na uzalishaji wa injini ya kitaifa.
Katika ukaguzi huo wa siku ya Jumatatu ulioendelea kwa muda wa masaa matatu na kuhudhuriwa na mawaziri kadhaa na wakurugenzi wa sekta mbalimbali za viwanda na madini, wataalamu wa kiwanda hicho walitoa maelezo na ufafanuzi kuhusu mwenendo wa uzalishaji kiwandani hapo.
Moja ya sehemu zilizotembelewa na Kiongozi Muadhamu ni sekta ya uzalishaji wa injini ya kitaifa ya magari. Ayatullah Khamenei amekagua na kupewa maelezo kuhusu uzalishaji wa sehemu mbalimbali za injini hiyo na majaribio iliyofanyiwa.
Moja ya sehemu muhimu zilizokaguliwa na Kiongozi Muadhamu ni uzalishaji wa injini ya kitaifa ya dizeli ya magari. Katika sehemu hii Ayatullah Khamenei ameshuhudia injini ya kwanza ya kitaifa ya dizeli iliyotengenezwa na wataalamu wa Iran ambayo inatumiwa katika treni, zana za baharini, vituo vya kuzalisha umeme na viwanda.
Maonyesho hayo pia yalijumuisha aina mbalimbali za injini za kitaifa za magari na injini zinazotumia gesi.
Sehemu nyingine ya maonyesha hayo ilikuwa ya utumiaji wa teknolojia ya kisasa hususan ile ya nano katika kubuni na kutengeneza vipuri.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia alikagua sehemu ya uzalishaji wa magari katika kiwanda hicho.
Baadaye Ayatullah Ali Khamenei alihutubia hadhara ya wakurugenzi na wataalamu wa sekta ya viwanda akiashiria umuhimu wa kujitegemea na kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiviwanda katika ustawi wa Iran ya Kiislamu na akasema, harakati ya taifa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda inapiga hatua za maendeleo. Amesisitiza kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya viwanda hapa nchini, kuna udharura wa kuwepo harakati kubwa zaidi katika sekta hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na ufuatiliaji mkubwa zaidi kwa kutegemea elimu na sayansi na kupandisha juu ubora wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ziara yake ya kukagua kiwanda hicho ni harakati inayolenga kusisitiza juu ya umuhimu wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya taifa. Amesema kuwa awali kulikuwepo fikra hatari na potofu inayodai kuwa kuna mgongano na ukinzani baina ya maisha ya kimantiki na ustawi kwa upande mmoja na kushikamana na thamani za kiroho, kimaadili na kidini kwa upande mwingine, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebatilisha dhana hiyo potofu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya masuala ya kiroho na sayansi na akasema: "Tunaweza kuishi maisha ya mantiki, maendeleo na ustawi na wakati huo huo tukashikamana na thamani za kimaadili na maamrisho ya dini." Amesisitiza kuwa wadau na wakurugenzi wa sekta ya viwanda wanapaswa kuwa dhihirisho la uhakika huo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya viwanda hapa nchini yana thamani kubwa na akaongeza kuwa: "Maendeleo hayo ni mwanzo wa njia na tunapaswa kujitegemea katika nyanja zote za viwanda na kuegamia fikra na ubunifu wa Kiirani."
Akiashiria uwezo wa Iran ya Kiislamu kwa ajili ya maendeleo na kujitegemea katika nyanja mbalimbali za viwanda, Ayatullah Ali Khamenei amesema matokeo ya harakati ya sasa ya wananchi wa Iran na vipawa vikubwa vya kizazi cha vijana wa Kiirani ni ustawi wa kiviwanda wa Iran katika ulimwengu wa Kiislamu, suala ambalo bila shaka litakaribishwa na ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia amekumbusha nukta kadhaa kuhusu sekta ya viwanda hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu sera za biashara kwa shabaha ya kuzuia uingizaji ovyo wa bidhaa nchini. Amesema kuwa kupatikana bidhaa kwa wingi na kwa bei rahisi ni jambo zuri lakini suala muhimu zaidi ni ustawi wa viwanda vya ndani ya nchi; kwa msingi huo mlango wa kuingizwa bidhaa za nje nchini haupaswi kufunguliwa ovyo kwa visingizio ambavyo aghlabu yao havina msingi wowote.
Ayatullah Khamenei ameelezea kutoridhishwa kwake na sera za uingizaji wa magari kutoka nje na baadhi ya maamuzi yaliyochukuliwa katika sekta hiyo na akasema, kwa ujumla falsafa na mantiki inayotumiwa kwa ajili ya kuzidisha uagizaji wa bidhaa kutoka nje ni kupeleka juu ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, lakini lengo hilo linaweza kufikiwa kwa kutumia njia bora zaidi, miongoni mwao ikiwa ni kuweka vigezo na sera makhsusi za kuboresha viwango vya bidhaa zinazozalishwa ndani.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutumia sayansi, elimu na uhakiki katika sekta ya viwanda na akasema, suala la kuwepo mfungamano wa karibu kati ya sekta ya viwanda na vyuo vikuu lina umuhimu mkubwa na kunapaswa kuwepo uhusiano madhubuti kati ya sekta hizo mbili ili kuweza kufikia ustawi na maendeleo.
Vilevile amesisitiza juu ya udharura wa kuuzwa nje bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na akasema kuwa sehemu zote za sekta ya viwanda zinapaswa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kuuzwa nje ya nchi na taasisi mbalimbali za serikali zinapaswa kufanya juhudi kubwa za kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa hizo.
Amezungumzia pia mtazamo wa dini ya Kiislamu kuhusu udharura wa kulindwa mazingira na akasisitiza juu ya wajibu wa kulindwa viwango vya taasisi za kulinda mazingira hususan katika sekta ya uzalishaji wa magari. Amesema ili kuweza kufikia ustawi na maendeleo katika sekta ya viwanda kunahitajika juhudi na kazi kubwa na endelevu, kwani mustakbali wa nchi na taifa la Iran umo katika uchapakazi na ufuatiliaji wa kudumu wa wadau na wakurugenzi wa sekta ya viwanda.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa serikali ya sasa ni serikali ya wachapakazi, yenye hima kubwa na moyo wa upendo na kwamba kwa sasa kuna mazingira bora zaidi kwa ajili ya kazi na juhudi kubwa katika sekta mbalimbali hususan viwanda.
Ayatullah Ali Khamenei amesema bongo na vipawa vikubwa vya Wairani sambamba na kuchapakazi bila ya kusita kunatayarisha mazingira mazuri kwa ajili ya ustawi na maendeleo. Ameongeza kuwa hii leo Iran ya Kiislamu inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi kadhaa duniani zinazoongoza katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia kutokana na hima kubwa, ubunifu, bidii na kujiamini kwa tabaka la vijana, na kwamba harakati hii inapaswa kuendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Madini wa Iran Muhandisi Mehrabian alitoa ripoti fupi kuhusu sekta ya viwanda hapa nchini na akasema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita nafasi ya Iran katika uga wa kimataifa imeboreka zaidi katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa mama kama chuma cha pua, alumini, shaba nyekundu, saruji na magari kutokana na ongezeko la uzalisha wa bidhaa hizo. Amesema kuwa sekta ya viwanda imestawi kwa asilimia 67 katika chati ya ustawi wa kiuchumi wa taifa.
Vilevile Waziri wa Viwanda wa Iran amesema kuwa uuzaji wa magari yaliyotengenezwa hapa nchini umeongezeka kwa kiwango kikubwa na akasisitiza kuwa uzalisha wa bidhaa hizo unazingatia utaalamu wa wasomi wa Kiirani, viwango vya kulinda mazingira na suala la kuuza nje bidhaa hiyo.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi wa kuzalisha injini ya taifa Muhandisi Mir Saliim amesema kuwa utengenezaji wa injini hiyo umechukua kipindi cha miaka 12 na kusisitiza kuwa awamu zote za kubuni na kutengeneza injini hiyo zimefanywa na wataalamu na wasomi wa ndani wakishirikiana na vituo vya vyuo vikuu. Muhandisi Mir Saliim amesema utengenezaji wa injini kubwa ya dizeli hapa nchini ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya wataalamu na wasomi wa Kiirani.
555826
captcha