IQNA

16:41 - September 02, 2010
Habari ID: 1986019

Kujifunza Qur'ani, mila na utamaduni muhimu zaidi barani Afrika

Naibu Mkuu wa taasisi ya kimataifa ya Jamiatul Mustafa (saw) anayeshughulikia masuala ya kimataifa amesema kuwa kujifunza, kusoma na kuhifadhi Qur'ani nzima ni miongoni mwa utamaduni na mila muhimu zaidi miongoni mwa Waislamu wa bara la Afrika.

Akizungumzia suala hilo katika kikao cha 'Qur'ani katika Upeo wa Kimataifa, Bara la Afrika' kilichofanyika siku ya Jumatano alasiri katika maonyesho ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu mjini Tehran, Hujjatul Islam wal Muslimeen Abdul Majid Hakimullahi amesema kuwa kuna mambo kadhaa ya kuvutia miongoni mwa Waislamu wa bara la Afrika kuhusiana na Qur'ani, moja ikiwa ni usomaji wa kitabu hicho kitakatifu. Amesema Waislamu Waafrika daima wako katika hali ya kusoma Qur'ani Tukufu, kwa maana kuwa ima wamehifadhi au wanatenga muda mrefu kwa ajili ya kusoma kitabu hicho kitukufu. Kwa kawaida huchukua masaa mengi kabla ya alfajiri kusoma Qur'ani.
Hakimullahi amesema kuwa mafunzo na usomaji wa Qura'ni una nafasi maalumu na muhimu miongoni mwa Waislamu Waafrika na kwamba huwapeleka watoto wao katika madrasa ili kujifunza kitabu hicho kitakatifu kabla ya kuhitimu umri wa kuingia katika shule za kawaida. Amesema watoto hao husoma na kujifunza Qur'ani katika mazingira magumu sana na kwamba mara nyingine hukosa hata mkeka wa kuketia darasani.
Hujjatul Islam Hakimullahi amesema si rahisi kupata familia ya Kiislamu barani Afrika ambayo haina watu wawili, watatu au hata zaidi ambao hawajahifadhi Qur'ani nzima. Amesema jambo jingine la kuvutia miongoni mwa Waislamu Waafrika ni kuwa wanawaheshimu sana watu waliohifadhi Qur'ani na hulichukulia jambo hilo kuwa wajibu kwao.
Hujjatul Islam Hakimullahi amesema jambo jingine la kuvutia miongoni mwa Waislamu wa Afrika kuhusiana na Qur'ani tukufu ni kuwa kila baada ya muda fulani husoma na kukamilisha Qur'ani tukufu katika kipindi maalumu kilichoainishwa pamoja na tafsiri za aya zake takatifu, na kisha kuandaa karamu na sherehe kubwa mwishoni mwa kila kisomo. Ameendelea kusema kuwa watu wa Afrika, ambao wengi ni Waislamu, wamekuwa wakizingatia sana Qur'ani tokea zama za kale kwa kadiri kwamba licha ya kuwepo matatizo ya umasikini na ukandamizaji wa wakoloni dhidi yao lakini wamekuwa wakizingatia misingi na mafundisho ya dini bila kuathiriwa na misukosuko ya maisha. Amesema alama, nara, dalili na madhihirisho ya Uislamu yanaonekana zaidi katika bara hilo kuliko maeneo mengine ya dunia.
Amesema, wakati wa kuadhiniwa na kuanza swala za kila siku, watu huacha kazi zao mara moja kwa lengo la kushiriki kwenye swala hilo za jamaa. Amesisistiza kwamba utamaduni wa watu wa Afrika umechanganyika na kufungamana kikamilifu na mafundisho ya Uislamu, na kwamba hawako tayari kwa njia yoyote ile kuachana na mafundisho ya dini yao.
Ameashiria hatua ya Mtume Mtukufu (saw) ya kutuma kundi la kwanza la Waislamu huko Habasha, Ethiopia ya leo, ili liwasilishe ujumbe wake kwa mfalme wa nchi hiyo, kuwa iliyo na siri kubwa. 646557
captcha