Mpango wa kujengwa msikiti huo ulipitishwa siku ya Ijumaa katika mkutano wa mameya wote wa maeneo mbalimbali ya Copenhagen ambapo waliupitisha kwa kura 45 dhidi ya kura tatu zilizopinga.
Akizungumzia jambo hilo katika mkutano wa waandishi habari, Bo Asmus Keldgaard, mkuu anayesimamia masuala ya kijani kibichi ya mji huo amedai kuwa uhuru wa kuabudu ni moja ya misingi muhimu ya Denmark na kwamba kila eneo lililo na kanisa linapasa pia kuwa na msikiti. Amesema ikiwa ni dini ya pili iliyo na wafuasi wengi nchini Denmark, Uislamu una wafuasi wapatao 50,000 katika mji wa Copenhagen tu na kwa hivyo wanahitaji kuwa na sehemu ya kutekelezea ibada zao.
Pendekezo la kujengwa msikiti huo lilitolewa na kukubaliwa na viongozi wa serikali ya nchi hiyo mwaka 1992 lakini makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka yalipinga vikali ujenzi wa msikiti huo, jambo lililopelekea kuakhirishwa ujenzi wake. Hatimaye mwaka 2005 na baada ya kuchapishwa nchini humo vikatuni vya kumvunjia heshima Mtume Mtukufu (saw) wimbi la chuki dhidi ya Uislamu liliongezeka nchini na hivyo kufunikwa kabisa suala la ujenzi wa msikiti uliotajwa.
Hata hivyo mwaka huu Waislamu walihuisha na kufuatilia kwa karibu ujenzi wa msikiti huo, jambo ambalo hatimaye limepitishwa hivi karibuni kwa wingi wa kura na baraza la mameya wa Copenhagen. 647739