Kwa mujibu wa gazeti la Saudi Arabia la al-Iqtiswaadiyya, sherehe hiyo ambayo imekuwa ikifanyika tarehe 3 Oktoba kila mwaka imekuwa ikifanyika nchini humo tokea mwaka 1997 kwa mnasaba wa kuungana Ujerumani mbili za Magharibi na Mashariki.
Katika siku hiyo Waislamu walio wachache nchini Ujerumani huwakaribisha misikitini wafuasi wa dini nyinginezo za nchi hiyo. Waislamu hujaribu kuwafahamisha wenzao wasiokuwa Waislamu mafundisho ya Kiislamu kupitia hotuba mbalimbali.
Akibainisha suala hilo, Ali Kizilkaya, mwanachama wa baraza hilo la uhusiano amesema kuwa, katika siku hiyo ya tarehe 3 Oktoba, milango ya misikiti 427 ya Ujerumani itakuwa wazi kwa shabaha ya kuwakaribisha wafuasi wa dini nyinginezo za Ujerumani ili wapate kufahamishwa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Amesema lengo la kuchaguliwa siku ya kuungana Ujerumani mbili kuwa siku ya kufanyika sherehe hiyo ni kusisitizwa umuhimu wa suala la wafuasi wa dini tofauti nchini Ujerumani kuishi pamoja kwa amani. 661542