Bahara Abdu al-Latif, mwanamke mwanafikra na mtafiti wa Iraq amesema kuwa kuchafuliwa jina la dini tukufu ya Kiislamu katika nchi za Magharibi kunatokana na Wamagharibi kutoifahamu vyema dini hiyo tukufu na mafundisho yake.
Akizungumza katika kikao cha nne cha kimataifa kinachojadili masuala ya wanawake huko Madrid nchini Uhispania, Abdu al-Latif amesema kuwa wanawake wa Kiislamu wanapaswa kushirikishwa vilivyo katika harakati na mipango ya ustawi na maendeleo ya nchi zao.
Abdu an-Nur Barado, mwanafikra na msomi mwingine wa Malaysia amesema kuwa wasomi na wanafikra wa Kiislamu ambao wanashiriki katika kikao hicho wamefanya utafiti na kuandika vitabu vingi kuhusiana na nafasi ya mwanamke katika jamii, jambo ambalo amewasihi wananchi wa Uhispania kufanya juhudi za kuvisoma ili wapate kuelewa sura na mafundisho sahihi ya Uislamu kuhusiana na thamani za mwanamke katika jamii.
Washiriki wa kikao hicho vilevile wamechunguza hali ya mwanamke wa Kiislamu katika pembe mbalimbali za dunia na kusisitiza kuwa Uislamu unazingatia kwa kiwango kikubwa thamani na haki za binadamu na kwamba umebuni misingi na sheria madhubuti za kulinda haki na heshima ya mwanamke.
Kikao hicho cha kuchunguza masuala ya wanawake kwa mtazamo wa Kiislamu mjini Madrid kilimalizika hapo jana tarehe 24 Oktoba. 681225