Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA mjini Makka al Mukarramah, Kiongozi wa Msafara wa Mahujaji Wairani Hujjatul Islam Sayyid Ali Ghaziasghar amehutubu katika kikao hicho na kusema kuwa kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni suala muhimu. Amesema kufanyika makongamano mengi kuhusu suala la kuyakurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu ni jambo linaloashiria kuwepo makubaliano miongoni mwa madhehebu ya Kiislamu kuhusu umuhimu wa kukurubiana. Amesema siri ya kudumu Uislamu duniani ni kutii amri ya Mwenyezi Mungu anaposema, "Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane". Al Imran 3:103
Amesema mgawanyiko na mifarakano ni jambo linaloharibu heshima ya Waislamu na kutoa mwanya kwa maadui kuwatawala. Hujjatul Islam Sayyid Ali Ghaziasghar amesisitiza kuwa Waislamu wana nukta nyingi za pamoja ikiwa ni pamoja na imani ya Mungu Mmoja, Qur'ani Tukufu, Mtume Muhammad SAW na Ahul Bayt AS. amesisitiza kuwa 'Iwapo Waislamu watazingatia nukta zao za pamoja, basi wanaweza kuwa na ushawishi mkubwa duniani.
Aidha mwanazuoni huyo wa Iran amesema kuwa maulamaa wa Kiislamu wanapaswa kusimama na kukabiliana na watu wenye misimamo mikali ya kufurutu mipaka na wanaoeneza itikadi potofu zisizofungamana na Qur'ani Tukufu.
Kati ya waliohutubu katika kongamano hilo ni wawakilishi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Mkuu wa Msafara wa Hija wa Iraq Sheikh Ahmad Khalaf Jawad, Mkuu wa Msafara wa Hija wa Uturuku Sheikh Shakur Uz Budagh pamoja na wawakilishi wa mahujaji wa Misri, Pakistan na Nigeria. 692869