Kwa mujibu wa shirika la habari la Ufaransa AFP, Mufti Gaynutdin ameashiria baadhi ya vitendo vilivyotekelezwa dhidi ya Uislamu nchini humo katika miezi ya hivi karibuni na kuwataka viongozi wa serikali, dini na vyombo vya habari vya Russia kuzidisha juhudi zao za kukabiliana na wimbi la kuchochea hofu na chuki dhidi ya mafundisho ya Kiislamu katika jamii ya nchi hiyo.
Amewataka viongozi wa kidini na serikali kukemea kwa maneno makali vitendo kama vile vya kushambuliwa Waislamu, nara za kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu pamoja na kukosewa heshima matukufu ya Kiislamu kwa sababu jambo hilo amesisitiza, linaonyesha kuongezeka kwa vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu kwa kiwango kisichokubalika katika jamii ya Russia.
Ravil Gaynutdin amevitaka vyombo vya habari kutochochea hisia za utaifa na ubaguzi katika tabaka la vijana wa nchi hiyo kwa sababu vijana wa Kiislamu pia wana matarajio ya kuishi katika mazingira ya utulivu na amani nchini humo. 713320