IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yaanza Iran

13:24 - January 09, 2011
Habari ID: 2061031
Awamu ya Tatu ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yanaanza leo Januari tisa katika mji mtakatifu wa Mash'had Kaskazini Mashariki mwa Iran.
Sherehe za Ufunguzi wa mashindano hayo zinatazamiwa kufanyika baada ya Swala za Magharibi na Ishaa katika ukumbi wa mikutano wa IRIB karibu na Haram Takatifu ya Imam Ridha AS.
Wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka nchi 40 duniani na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran watashiriki katika mashindano hayo ya siku tatu ya Qur'ani Tukufu ambayo yatakuwa katika vitengo ya hifdhi na qiraa.
Majaji katika mashindano hayo ni wataalamu wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu wakiwemo Ustadh Farajullah Shadhili kutoka Misri, Ustadh Mazar As-Sharif kutoka Iraq, Sheikh Ridhwan Darwish kutoka Syria na Sheikh Ali al-Musalamani kutoka Lebanon.
Wageni mashuhuri katika mashindano hayo ni qarii maarufu wa Misri Ustadh Ahmad Ahmad Noaina na vilevile Utadh Ali Burak kutoka Uturuki na Sheikh Fakhruddin Sarumpaet Siddique.
Pembizoni mwa mashindano hayo ya siku tatu kutakuwa na vikao viwili vya kielimu kuhusu “Chuki na Uhasama Dhidi ya Uislamu” na vilevile”Kuelekea katika Maisha ya Qur'ani”.
Mikutano hiyo itahudhuriwa na Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu Dkt. Muhammad Bakir Khorramshad na Naibu Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu Sheikh Hamid Muhammadi ambaye anasimamia masuala ya Qur'ani katika wizara hiyo.
Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yameandaliwa na Jumuiya ya Harakati za Qur'ani ya Wanachuo wa Iran (inayofungamana na Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu) kwa ushirikiano wa Idara ya Mkuu wa Mkoa wa Khorasan Razavi na taasisi kadhaa za harakati za Qur'ani na utamaduni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 725739
captcha