Taarifa zinasema Dkt. Al Shadhili ambaye alikuwa pia Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Qur’ani Misri amerejea kwa Mola wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Kijeshi ya Al Jalal Al Askari mjini Cairo.
Ustadh al Shadhili alizaliwa mwaka 1948 katika kijiji ya cha Armania katika mkoa wa Beheira na ameaga dunia katika siku ya 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani akiwa na umri wa miaka 69. Mnamo mwaka 1971 alijiunga na Chuo cha Qiraa ya Qur’ani Misri na alihitimu mwaka 1979. Katika mwaka 1980, aliamua kuendeleza masomo yake na kujiunga na Kitivo cha Msomo ya Kiarabu na Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Al Azhar na kuendelea hadi alipopata shahada ya Uzamifu au Phd mwaka 2004. Katika kipindi cha masomo yake alikuwa akiendeleza harakati zake za Qur’ani.
Ustadh Al Shadhili alikuwa pia muadhini wa Al Azhar na qarii rasmi wa Radio na Televisheni ya Misri. Aidha alikuwa jaji katika mashindano mengi ya kimataifa ya Qur’ani duniani. Mwaka 2011 alikuwa jaji katika Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qurani ya Wanachuo Waislamu yaliyofanyika katika mji wa Mash’had nchini Iran. Aidha amewahi kualikwa kusoma Qur’ani katika miji mbali mbali ya Jamhuri ya Kiislamu Iran. Ustadh Al Shadhili alihimiza sana umoja wa Waislamu na ukuruba wa madhehebu za Kiislamu.
Wiki iliyopita Ustadh Al Shadhili alikuwa nchini Austria kufuatia mwaliko wa Waislamu nchini humo ambapo mbali na kuswalisha katika siku za kwanza za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pia alikuwa qarii wa Qur’ani Tukufu katika siku hizo kabla ya kurejea Misri siku tano zilizopita. Mazishi ya Ustadh Farajullah Al-Shadhili yanafanyike leo Jumanne katika kijiji alikozaliwa cha Armania. Tunamuomba Allah SWT amghufurie dhambi zake na amjaalie sehemu bora katika janna.
Bonyeza hapa kusikiliza tajwidi ya Marhum Ustadh Al Shadhili.