Aidh al-Qarani, mwanazuoni wa Kisuni wa Saudi Arabia ameutaka umma wa Kiislamu kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kuzuia na kukomesha fitina za kimadhehebu na hasa kati ya wafuasi wa makundi mawili muhimu ya Kiislamu ya Shia na Suni.
Sheikh Aidh al-Qarani amesisitiza kwamba umma wa Kiislamu unahitaji kuchukua uamuzi muhimu wa kisiasa wa kuondoa kabisa fitina kati ya makundi mawili haya na kila kundi kuruhusiwa kuendesha shughuli zake za kimadhehebu kwa uhuru kamili.
Amesema Mwenyezi Mungu hajawataja Waislamu kwa majina ya Kisuni wala Kishia bali amewataja wote kuwa ni Waislamu.
Mwanazuoni huyo wa Kisuni amewataka viongozi wa nchi za Kiarabu kuingilia kati na kusuluhisha kati ya makundi mawili haya ya Kiislamu na kuzima moto wa fitina unaowaka baina yao. Ametaka kuenezwa kwa misimamo ya wastani miongoni mwa Waislamu na kuwataka pia Waislamu wa Misri waishi kwa amani na wafuasi wa dini nyinginezo. 727385