IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo yakamilika

13:14 - January 12, 2011
Habari ID: 2063578
Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qurani ya Wanachuo Waislamu yalimalizika Januari 11 usiku katika mji wa Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA mjini Mash'had sherehe za kufunga mashindano hayo zilijumuisha kisomo cha Qur'ani cha maustadhi mashuhuri wa Misri Abul Ainain Shuaisha na Farajullah Shadhli.
Sherehe hizo zilianza kwa wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kufuatiwa na kisomo cha Qur'ani cha mshindi wa kitengo cha kiraa Hamid Walizadeh wa Iran.
Baada ya hapo mwanaharakati mkongwe wa Qur'ani kutoka Iran Abbas Salimi alisoma mashairi yaliyofuatiwa na filamu fupi ya mashindano ya tatu ya wanachuo Waislamu.
Baada ya hapo kulikuwa na kisomo cha Ibtihal kutoka kwa Ridhwan Darwish Msyria ambaye pia alikuwa katika jopo la majaji. Kisomo hicho kilifuatiwa na ripoti fupi ya mashindano iliyosomwa na Issa Alizadeh katibu wa duru hii ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani.
Amesema sifa ya kipekee ya Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu ni kuwa yamefanyika karibu na Haram Takatifu ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Ridha AS jambo linaloashiria mshikamano mkubwa uliopo baina ya Qur'ani Tukufu na Watu wa Nyumba ya Mtume – Ahlul Bayt-AS.
Ameongeza kuwa wanafunzi kutoka nchi 40 duniani wameshiriki katika mashindano hayo chini ya nara ya 'Umoja wa Kiislamu kwa Msingi wa Qur'ani'. Amesema kuwa mashindano hayo yamehudhuriwa maustadhi bingwa wa Qur'ani kutoka Ulimwengu wa Kiislamu ambao walikuwa katika jopo la majaji.
Alizadeh aliashiria vikao vya kisayansi pembizoni mwa mashindano hayo na kusema vimehudhuriwa vizuri na washiriki.
Akigusia mipango ya siku za usoni ya Jumuiya ya Harakati za Qur'ani ya Wanachuo wa Iran (mwandalizi wa mashindano hayo), amesema kuna mpango wa kuasisi makao makuu ya kudumu ya mashindano hayo."Jumuiya hii pia inapanga kuanzisha Umoja wa Kimataifa wa Harakati za Qur'ani wa Wanachuo Waislamu".
Baada ya hotuba ya Alizadeh, Muhammad Salim al Ghazali kutoka Indonesia ambaye alichukua nafasi ya tatu katika kitengo cha kuhifadhi Qur'ani alisoma Qur'ani kwa njia ya tarteel kisha Ustadh Mazar As-Sharif alisoma taarifa kwa niaba ya jopo la majaji.
Jopo hilo la majaji limeishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na viongozi wake kwa kuandaa mashindano hayo na kuyataja kuwa hatua kubwa ya kuleta umoja wa Kiislamu, kustawisha mwamko miongoni mwa vijana Waislamu na kuwahimiza waelekee katika akhlaqi njema na umaanawi.
Nafasi ya kwanza katika uwanja wa hifdhi ya Qur’ani nzima imechukuliwa na mwakilishi wa Iran Muhammad Khatibi akifuatiwa na wawakilishi wa Libya Badruddin Abdulhakiim ambaye ameshika nafasi ya pili na Muhammad Salim Ghazali kutoka Indonesia aliyepata nafasi ya tatu. Katika kiraa ya Qur’ani Tukufu mwakilishi mwingine wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hamid Waliizadeh ameshika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Sayyid Hamidullah Hashimi kutoka Afghanistan na Sayyid Thamaruddin Sanadov kutoka Tajikistan aliyepata nafasiu ya tatu.
Washindi wa kwanza wa mashindano hayo wametunukiwa zawadi ya dola elfu kumi kila mmoja, nafasi ya pili dola elfu nane na nafasi ya tatu dola elfu tano. Washindi hao wote pia wametunukiwa loho na nishani ya mashindano ya sasa ya Qur’ani ya wanachuo wa Kiislamu.
Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qurani ya Wanachuo Waislamu yalifanyika Mash'had kuanzia Januari 9-11 na kuwashirikisha maqari na mahafidh kutoka nchi 40 duniani.
729004
captcha