Kwa mujibu wa gazeti la Arab News, Swalih bin Ibrahim Babueir Naibu Katibu Mkuu wa Wamy anayeshughulikia masuala ya utendaji amesema kwamba mashirika mawili hayo yameafikiana kuongeza ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali za shughuli zao ukiwemo ubadilishanaji vitabu na majarida. Amesema mashirka hayo pia yatabuni kamati ambayo itakuwa ukijihusisha na masuala ya kuratibu shughuli za ushirikiano wa pande mbili.
Katika upande wake, Said Sharaf ad-Deen Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lililotajwa la misaada ya Kiislamu la Uingereza ameashiria uzoefu wa miaka 20 wa shirika hilo katika utoaji misaada katika nchi 70 za dunia na kuongeza kuwa shirika hilo limepata mafanikio makubwa katika kupunguza umasikini katika nchi hizo.
Amesema shirika hilo lina malengo matatu muhimu ambayo ni kupunguza machungu ya watu masikini, kutoa suhula za mafunzo na masomo na kuwasaidia watu wanaohitajia misaada ili kuwanufaisha na mahitaji ya kimsingi maishani.
Amesema katika wiki za hivi karibuni shirika hilo limetiliana saini na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC na Benki ya Ustawi ya Kiislamu kwa shabaha ya kufikiwa lengo la pamoja la kupunguza machungu ya watu katika nchi za Kiislamu wakati wa kutokea mabalaa ya kimaumbile. 754772