Kwa mujibu wa tovuti ya PRNewsWire, wiki iliyopita mwanamke mmoja wa Kiislamu katika mji huo aliona maandishi ya matusi yakiwa yameandikwa kwenye ukurasa mmoja wa Qur'ani na kuwekwa kwenye kioo cha gari lake, alipokuwa akiingia kwenye gari lake akitokea sokoni.
Mwanamke huyo mvaaji hijabu na aliye na uraia wa nchi mbili za Misri na Marekani aliwasiliana kwa njia ya simu na Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR na kulibainishai tukio hilo huku akitaka lifuatilie jambo hilo kupitia vyombo vya polisi.
Maafisa wa baraza hilo wamewataka polisi kukabiliana vikali na vitendo vya kukosewa heshima matukufu ya Kiislamu ambavyo wanasema vimeongezeka sana katika jimbo la California kutokana na uungaji mkono wa baadhi ya viongozi wa serikali wa jimbo hilo kwa wafanyadharau dhidi ya matukufu ya Kiislamu.
Siku chache zilizopita pia, Waislamu wawili wa mji wa Sacramento katika jimbo hili walipigwa risasi na watu wasiojulikana.
Kwa ujumla Waislamu wanaoishi katika mji huo wanakabiliwa na vitendo mbalimbali vya dharau kutoka kwa Wamarekani wenye misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu.
Baraza la CAIR ambalo liliasisiwa mwaka 1994 mjini Washington ni taasisi kubwa zaidi inayotetea haki za kiraia za Waislamu nchini Marekani, na hivi sasa lina matawi katika majimbo karibu yote ya Marekani. Lengo jingine la baraza hilo ni kuarifisha sura halisi ya Uislamu kwa Wamarekani na kuwashirikisha Waislamu katika nyanja mbalimbali za maendeleo nchini humo. 763024