IQNA

Nowruz chimbuko la umaridadi wa maumbile, turathi ya dunia

10:33 - March 27, 2011
Habari ID: 2098273
Jumatatu 21 Machi ilisadifiana na tarehe Mosi Farvardin mwaka 1390 Hijria Shamsia ambayo kwa lugha ya Kifarsi inajulikana kama siku ya Nowruz ambayo sasa inaadhimishwa kimataifa. Siku ya Nowruz imewekwa katika orodha ya Shirika la Utamaduni, Sayansi na Elimu UNESCO ya turathi za dunia.
Kwa mara nyingine, adhama na uwezo usio na kifani ya Mwenyezi Mungu unadhihirika katika msimu maridadi kabisa wa mwaka. Kwa mara nyingine msimu wa machipuo umewadia ukiwa umeandamana na umaridadi wa aina yake wa mwanaadamu na kutoa shukrani kwa Mola muumba. Hivi sasa kuna ari mpya katika maumbile asilia, na hii ni kwa sababu ni wakati wa kunawiri na kuibuka upya. Jua lenye mng'aro wa kipekee linachomoza mbinguni. Mchanga unatoa harufu mpya na maua yanaibuka yakiwa na rangi anuai za kuvutia katika matawi ya miti na hayo yote yanateka macho ya kila mtazamaji. Ardhi imepambwa kwa kijani kibichi na mimea ya msimu yenye rangi za kuvutia na hivyo msimu unaanza kwa ari mpya.
Sauti ya uhai katika mwanga wa msimu wa machipuo inaupa moyo wa mwanadamu utulivu na furaha na kuandamana naye katika sherehe za maumbile asilia. Mwanaadamu anaketi na kutafakari katika mandhari isiyo na kifani ya maumbile huku akiburudika kwa kutazama adhama ya kuzaliwa upya maumbile asilia. Hii ni kwa sababu kila mwenye hekima huwa daima anataka kudiriki uhakika na hutizama ulimwengu kama sehemu ya kupata funzo na ibra. Mwenyezi Mungu katika Qurani Tukufu Sura Ali Imran aya ya 190 anakumbusha kuhusu nukta hii kwa kusema: "Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko ishara kwa wenye akili,"
Kile kinachojiri mwanzoni mwa msimu wa machipuo humfanya mwanaadamu kuwa mwangalifu. Uhai ambao hurejea baada ya kudidimia wakati wa msimu wa baridi huakisi ukweli kuwa Mwenyezi Mungu SWT ana uwezo wa kumhuisha mwanaadamu kutoka mauti katika ulimwengu mwingine. Katika sehemu ya aya ya 5 na 6 ya Sura al Hajj katika Qurani Tukufu tunasoma kuwa; "Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapoyateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri. Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu".
Katika maisha yake, mwanaadamu anahitajia maktaa na misimu mipya ili kwa uzoefu aliopata huko nyuma aanze harakati mpya. Wananchi wa Iran katika mwanzo wa msimu huu mpya wanamuomba Mwenyezi Mungu kwamba sambamba na uhai mpya wa maumbile asilia nao pia wapate mabadiliko. Hii ndiyo sababu mwanzo wa kuingia mwaka mpya wa Hijria Shamsia wao huomba dua ifuatayo:
يا مقلّب القلوب و الأبصار، يا مدبّر اللّيل و النّهار، يا محوّل الحول و الأحوال، حوّل حالنا الی احسن الحال.
“Ewe Mwenye kubadilisha nyoyo na macho,
Ewe mwenye kuratibu usiku na mchana,
Ewe mwenye kuzungusha zama na hali,
Badilisha hali yetu iwe katika hali bora zaidi.
Katika dua hii, ulimwengu una mabadiliko ya kina na yenye upana mkubwa. Kwa hakika, ili dunia ibakie ni lazima ishuhudie mabadiliko ya kimsingi. Kwa hivyo tunashuhudia namna maumbile asilia duniani yanavyokumbwa na mabadiliko na kuibua umaridadi wenye kuvutia na kwa misingi yake yote inamtukuza na kumhimidi Mwenyezi Mungu. Iwapo tutazingatia kidogo tu, tunaweza kusikia maumbile asilia yakimshukuru Mwenyezi Mungu. Sauti ya upepo mwanana unaoashiria tauhidi pamoja na matawi ya miti yanayosukumwa na upepo kulia na kushoto ni kana kwamba yanashuhudia adhama ya muumba wa dunia. Mvua za msimu wa machipuo zinasafisha na kutakasa ardhi na mimea ya rangi anuia kuchipua.
Mwanaadamu ni sehemu muhimu ya mabadiliko makubwa ya mazingira wakati wa kuanza majira ya machipuo.
Dua ambayo mja anamuomba Mola wake wakati wa kuingia mwaka mpya wa Hijria Shamsia ambao huwa ni mwanzo halisi wa machipuo huwa dua yenye mafunzo ya tauhidi. Dua hii inaashiria kuwa mabadiliko yote ya maumbile asilia hutokana na uwezo na hekima ya Mwenyezi Mungu. Ni Yeye peke yake aliye na uwezo wa kukidhi maombi yote ya mwanaadamu.
Sambamba na maua yenye manukato mazuri wakati msimu wa machipuo unaponawiri, mwanaadamu anashuhudia na kufurahia uzuri na utakasifu uliopo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei anasema: “Nouruz ni siku mpya katika historia ya mwanaadamu na hali mpya katika maisha ya wanaadamu…Noruz ni siku ambayo wewe kwa amali zako, kwa yanayojiri, unaifanya siku hiyo kuwa mpya”.
Katika mwaka mpya, tunaipokea siku ya Nouruz na machipuo katika hali ambayo Waislamu wa eneo la Mashariki ya kati wameanzisha harakati ya mabadiliko mapya. Muelekeo waliochukua watu wa eneo ni wa kuupa thamani uanaadamu, kutaka uhuru na uadilifu. Watu wa Tunisia, Misri, Bahrain, Yemen, Libya n.k wameamka kupinga muundo wa tawala za nchi zao ambazo zinaenda kinyume na ubinaadamu na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Wananchi hao wameamka ili ku’ngoa mizizi ya dhulma na ukosefu wa uadilifu na kupanda mbegu za miti ya kijani kibichi itakayo kuwa na matawi ya uhuru, ukuruba na utakasifu ili iweze kutoa harufu nzuri ya umaanawi na tauhidi katika mitaa yao.
Hivi sasa katika nchi hizo baada ya msimu wa baridi kali, utegemezi wa mabeberu na dhulma kumetanda harufu nzuri ya machipuo ya maisha mapya na uhuru. Jua lenye mwanga linachomoza kote duniani na kutoa bishara za hali mpya yenye kusisimua. Ardhi inatoa harufu nzuri yenye joto la mwamko. Ndege wenye kuimba wanapaza sauti ya umoja na mapenzi. Kwa hakika Machipuo haya yanaweza kumletea mabadiliko mwanaadamu aliyekuwa ameghafilika na kusinzia. Hili linawezekana tu kwa sharti kuwa mwanaadamu ajiweke mbali na wingu jeusi la ghururi, kiburi, mifarakano na upotoshaji .Kujiweka mbali na hayo kutazuia machipuo kuwa huzuni.
Mpenzi msikilizaji, kwa vyo vyote vile kuingia mwaka mpya wa Hijria Shamsia yaani nouruz huandamana na mabadiliko katika maumbile asilia na huwa fursa kwa mwanaadamu naye pia kuwa na mabadiliko na marekebisho kwenye nafsi yake katika masuala ya kimaanawi na kidunia. Msomi mkubwa wa kidini na mfasiri wa Waislamu katika kitabu cha Kashful Asrar anaandika: 'Idi ni neno ambalo chimbuko lake ni kurejea. Kutokana na kuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu mja wake na mwanaadamu naye kwa utiifu wake anarejea kwa Mola wake muumba subhanahu wa taala.’ Hili linamaanisha kuwa mwanaadamu sambamba na usafi wa kidhahiri lazima awe ametakasika ndani ya nafsi yake. Aondoe kutoka moyoni mwake yote yasiyofungamana na Mwenyezi Mungu na awe mtenda amali njema na zinazofaa ili kwa njia hiyo royo na moyo wake ujae mwangaza na manukato mazuri.
Msimu maridadi wa machipuo na vivituio vyake vizuri ni fursa ya kufikia kiwango cha urafiki wa juu na wenye kunawiri. Katika siku hizi kote huwa kumeenea urafiki, ukuruba na mapenzi, na macho huwa na hamu ya kuona mwangaza. Kuwaheshimu wakubwa na wazee, kutembelea jamaa na kwa ujumla kutembeleana ni katika sunna za tangu jadi za Wairani katika siku hizi za Nouruz. Katika siku hizi tabasamu za kuvutia huwa zimetanda kote na kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW:
“Kutembeleana na kukutana hukuza urafiki katika nyoyo.”
Mpenzi msikilizaji Nouruz ni siku ya rangi za ukarimu, tabasamu zenye kupenya kwenye moyo na siku ya kuzika huzuni na chuki. Uislamu ni dini yenye utamaduni wa mshikamano, kupendana, tabasamu, tabia njema na ukarimu. Imam Ali anasema: “Muumini ni mtu ambaye uso wake ni wenye tabasamu na furaha na anaficha masaibu na huzuni yake.”
Kwa hivyo siku za kuanza msimu wa machipuo zinapaswa kuwa siku za kupeana zawadi ya kufurahisha nyoyo na kuimarisha na kuboresha urafiki wa marafiki na jamaa.
Imam Sadeq AS anasema: “Mwanzao wa Farvardin ni siku aliyoumbwa mwanaadamu, ni siku bora ya kuomba mahitajio na kujibiwa uliyoyataka, ni siku ya kupata elimu. Katika siku hii jisafishe vizuri na ukae ukiwa msafi vaa vazi bora zaidi. Jipake uturi na kisha mkumbuke Mwenyezi Mungu”
763332

captcha