IQNA

Eid al-Adha: Kutoka Mapokezi ya Kiibrahim hadi Mila za Kiislamu Leo

15:18 - May 27, 2026
Habari ID: 3482291
IQNA – Eid al-Adha, ambayo ni miongoni mwa sikukuu adhimu zaidi katika Uislamu, ni ukumbusho wa kisa cha kihistoria cha imani, taslimu (kujisalimisha kwa Allah), na kujitolea.

Katika tukio hili, Nabii Ibrahim (A.S) aligeuka kuwa kioo cha uja na utiifu katika mtihani mzito kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sherehe hizi zinaendelezwa hadi leo kupitia ibada ya Hija na katika utamaduni wa Kiislamu kama sikukuu iliyojaa hali ya kiroho na mshikamano wa kijamii.

Ibada na amali za  Hija katika Uislamu ni mfululizo matendo ya kiishara, ambapo kila moja ina mizizi ya kina ya kihistoria na kimaanawi. Miongoni mwa ibada hizo, maeneo ya Mina na Qurbani (uchinjaji) yana nafasi ya kipekee. Mina si kituo kikuu cha Hija pekee, bali katika mapokezi ya Kiislamu, inajulikana kama sehemu ambapo amali muhimu zaidi hutekelezwa baada ya Wuquf (kusimama) kule Arafat.

Qurbani pia ni moja ya nembo kuu za Hija, inayotukumbusha kisa cha Nabii Ibrahim (A.S) na mwanawe Ismail (A.S) na dhana ya kunyenyekea mbele ya amri ya Mola. Kuchunguza historia ya Mina na kutoa dhabihu hutujulisha uhusiano uliopo kati ya mila za kale za Kiarabu, mageuzi ya ibada baada ya kuja kwa Uislamu, na maana ya kidini na kijamii ya amali hii.

Mina katika Historia ya Uarabuni

Mina ni eneo lililo karibu na Makka ambalo kwa muda mrefu limekuwa likivutia watu wakati wa msimu wa Hija. Katika kipindi cha kabla ya Uislamu (Jahilia), Waarabu walifika maeneo ya jirani na Makka kutekeleza mila fulani za msimu, na Mina ilikuwa miongoni mwa vituo hivyo vilivyojulikana. Hata hivyo, katika kipindi hicho, mila za kidini za Kiarabu zilichanganywa na itikadi za kikabila, ushirikina (kuabudu masanamu), na mila za wenyeji. Kwa hivyo, Mina haikuwa na maana moja thabiti ya kidini kama ilivyo leo, bali ilitambulika kama sehemu ya jiografia ya kiibada ya Makka.

Kwa ujio wa Uislamu, Mina ilipata hadhi rasmi katika muundo mpya wa ibada ya Hajj. Katika maandiko ya Kiislamu, Mina ilitambuliwa kama mahali pa kurusha mawe (Ram-ul-Jamarat), mahali ambapo mahujaji hukaa wakati wa siku za Tashreeq, na mahali pa kuchinja. Hivyo, eneo hili lilibadilika kutoka nafasi ya kimila na msimu na kuwa sehemu iliyofafanuliwa vyema katika ibada za Kiislamu.

Uchinjaji (Qurbani) katika Mila za Kabla ya Uislamu

Kabla ya Uislamu, uchinjaji wa wanyama ulikuwa jambo linalojulikana miongoni mwa makabila ya Kiarabu. Mara nyingi uchinjaji huu ulifanywa ili kuyaridhisha masanamu, kutimiza nadhiri na haja, na kukamilisha mila za kikabila. Lakini amali hizi hazikuwa na muundo wa kumpwekesha Mungu (Tauhidi). Mahali pa kuchinjia pia palitofautiana kulingana na kabila, hekalu, au ibada maalum. Kwa mtazamo huu, Uislamu haukuondoa uchinjaji, bali ulibadilisha maana na mwelekeo wake: uchinjaji ulibadilika kutoka kwa tendo la kishirikina na kuwa ibada ya kimfumo ya kumpwekesha Allah (SWT).

Qurbani katika Uislamu na Uhusiano wake na Nabii Ibrahim

Katika Uislamu, Qurbani ina mizizi katika kisa cha Nabii Ibrahim (A.S). Kwa mujibu wa masimulizi ya Qur’ani, Ibrahim aliamriwa kumchinja mwanawe, lakini katika wakati wa mtihani, Mwenyezi Mungu alikubali utiifu wake na kubadilisha sadaka hiyo kuwa mnyama mkubwa. Masimulizi haya ndiyo msingi wa kiroho wa Qurbani katika Hajj.

Kwa hiyo, uchinjaji katika Uislamu si tu kuua mnyama; ni ishara ya utiifu kwa amri ya Mungu, kujikomboa kutoka katika pingu za matamanio ya nafsi, kujitolea, kunyenyekea, na kukuza mshikamano wa kijamii. Katika sheria za Kiislamu, nyama ya Qurbani hugawanywa kati ya mwenye kuchinja, jamaa zake, na mafaqiri, jambo ambalo linasisitiza mwelekeo wa kijamii wa ibada hii.

Nafasi ya Mina katika Ibada za Hija Baada ya Uislamu

Baada ya kutekeleza Wuquf kule Arafat na Mash’ar, mahujaji huelekea Mina. Huko, kurushwa kwa mawe (Jamarat) hufanyika, uchinjaji hufanywa, na mahujaji hutumia sehemu ya siku za Tashreeq hapo. Katika historia yote ya Uislamu, eneo hili limekuwa mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya Hija. Kadiri idadi ya Waislamu ilivyoongezeka, namna ya utekelezaji wa uchinjaji imepitia mabadiliko ya kiufundi, lakini misingi yake imehifadhiwa. Katika zama za sasa, uchinjaji unafanywa kwa mpangilio katika machinjio maalum karibu na Mina chini ya mifumo ya afya na utawala ili kudumisha nidhamu na kuzuia matatizo ya kiafya.

Mwelekeo wa Kihistoria na Kijamii wa Wajibu wa Qurbani

Mbali na upande wa kidini, Qurbani katika Hija ina mwelekeo wa kihistoria na kijamii. Katika jamii ya kale ya Kiarabu, uchinjaji wa wanyama ulikuwa ishara ya ukarimu, nguvu za kikabila, na wakati mwingine nadhiri ya kidini. Uislamu uliichukua mila hii na kuipa mwelekeo mpya, ukiunganisha na uadilifu wa kijamii na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.

Eid al-Adha, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 10 Dhul-Hijjah, ni kumbukumbu ya utayari wa Nabii Ibrahim (A.S) kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na unyenyekevu wake wa mwisho kwa Mwenyezi Mungu; masimulizi ambayo hatimaye yakawa ishara ya kudumu ya rehema na utiifu.

Katika mafundisho ya Kiislamu, Eid al-Adha inaenda sambamba na kilele cha ibada ya Hajj kule Makka na inachukuliwa kuwa siku maalum kwa Waislamu kote duniani kujikurubisha kwa Allah, kusaidia wenye shida, na kuimarisha vifungo vya kijamii. Uchinjaji wa wanyama, swala za Eid, kutembeleana kwa familia, na kuwajali walio duni ni miongoni mwa madhihirisho muhimu zaidi ya siku hii.

Leo hii, Eid al-Adha bado inadumisha nafasi yake kati ya Waislamu, na licha ya mabadiliko ya mitindo ya maisha, ujumbe wake wa kiroho na kijamii bado uko hai na una tija katika kuunganisha nyoyo za Umma wa Kiislamu.

3497620

captcha