IQNA

19:01 - May 18, 2011
Habari ID: 2124717

Takwa la wakazi wa Karbala kwa serikali ya Saudia ikarabati makaburi ya Baqii

Waombolezaji wa Ummul Banin mkewe Imam Ali (as) katika mji mtakatifu wa Karbala wameutaka ufalme wa Saudi Arabia uruhusu makaburi ya maimamu watoharibu wa Ahlul Beit (as) huko Baqii yakarabatiwe.

Huku wakifanya maombolezo katika mji huo mtakatifu hapo siku ya Jumanne kwa mnasaba wa kuwadia siku ya kukumbuka kifo cha mtukufu huyo, waombolezaji walikusanyika katika haram ya Imam Hussein (as) mjini Karbala na kuutaka utawala wa Saudia ushughulikie jambo hilo haraka iwezekanavyo na kuwataka Waislamu wa sehemu nyingine za dunia wafanye mikusanyiko na maandamano ya malalamiko ili kutoa mashinikizo dhidi ya utawala huo.
Wamesema makaburi hayo ya Baqii mjini Madina ambako wamezikwa Maimamu wa Ahlul Beit (as) pamoja na watukufu wengine wa Kiislamu yanapaswa kukarabatiwa na kujengewa makuba ili kuongeza nuru ya kimaanawi ya mji huo pembeni ya kaburi la Mtume Mtukufu (saw).
Ummul Banin alikuwa mke wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) aliyemuoa baada ya kuuawa shahidi mkewe wa kwanza ambaye ni binti ya Mtume Mtukufu Bibi Fatma az-Zahra (as). Japokuwa Ummul Banin hakuwa katika uwanja wa vita vya Karbala lakini wanawe wanne walipigana bega kwa bega na Imam Hussein (as) dhidi ya maadui wa Uislamu na kuuawa shahidi wakiwa pembeni ya mtukufu huyo. Bibi huyo mtukufu aliaga dunia tarehe 13 Jamadu Thani mwaka wa 64 Hijiria na kuzikwa upande wa Magharibi wa makaburi ya Baqii pembeni ya Maimamu watoharifu (as). 794084
captcha