Katika taarifa iliyotelewa Julai 7, Hizbullah imesema: “Misimamo ya Sheikh al-Azhar ni ya kimsingi kwani imekuja wakati ambao vibaraka wa Magharibi wanajaribu usiku na mchana kuzusha fitina miongoni mwa Waislamu”.
Harakati ya Hizbullah imesisitiza kuwa: “Misimamo ya Sheikh al-Azhar ni ishara ya mitazamo sahihi na mkondo wa hekima uliopata ilhamu kutoka kwenye fikra ya Tauhidi. Ni njia inayofunga mlango kwa kila anayetaka kuzusha mifarakano miongoni mwa Waislamu na kuyavunjia heshima matukufu yao”.
Hizbullah imesema misimamo ya Sheikh al-Azhar ndio njia pekee ya kupambana na maadui wa Waislamu.
Hivi karibuni Ahmad al Tayyeb Shekhe Mkuu wa Al Azhar alipinga hujuma ya propaganda dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia inayoenezwa na baadhi ya makundi yenye misimamo mikali. Aidha alikosoa kanali za televisheni za satalaiti ambazo zinawavunjia heshima Mashia. Sheikh Ahmad Tayyeb amesema: “Mashia ni sehemu isiyotenganika ya umma wa Kiislamu. Mashia na Masuni wanahitilafia tu katika baadhi ya masuala ya pembeni”.
Aidha hivi karibuni Sheikhe wa al Azhar alitangaza kuwa tayari Chuo Kikuu cha Al Azhar nchini Misri kuwapokea wanafunzi wa Kishia na kuwaruhusu Marajii wa Kishia kujiunga na Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu ya Al Azhar.
Sheikh Ahmad Tayyib alisema kuwa Al Azhar ni nyumba ya Waislamu na milango yake iko wazo kwa makundi na madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Amesisitiza kuwa 'Waislamu wa madhehebu ya Shia ni sehemu isiyotenganika ya umma wa Kiislamu na sisi tunaswali nyuma ya maimamu wa Kishia. Ameongeza kuwa madai kwamba Mashia wana Qur'ani nyingine tofauti na hii iliyoko ni uongo mtupu'.
821923