IQNA

15:22 - August 04, 2011
Habari ID: 2165042

Kupandishwa kizimbani dikteta Mubarak nchini Misri ni pigo kwa Wamagharibi

Kesi ya Hosni Mubarak dikteta aliyepinduliwa nchini Misri pamoja na wanawe wawili Gamal na Alaa imefanyika hadharani Jumatano tarehe 3 Agosti katika kituo cha akademia ya polisi pambizoni mwa mji mkuu Cairo.

Kusikilizwa mara ya kwanza hadharani kesi ya dikteta Mubarak ambaye aliwatawala wananchi wa Misri kwa mkono wa chuma kwa miaka 30, ni suala ambalo lenyewe lina umuhimu mkubwa. Hii ni kwa sababu, kupandishwa kizimbani dikteta huyo kunaweza kuwa funzo na tahadhari kwa watawala wengine wa nchi za Kiarabu, zinazokabiliwa na hali kama ya Misri. Aidha kupandishwa kizimbani Mubarak ni kutasababisha hasara kubwa kwa nchi za Magharibi ambazo zimekuwa zikimuunga mkono.
Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kupandishwa kizimbani Hosni Mubarak na wanawe wawili ni ushindi mkubwa kwa taifa la Misri. Kwa muda wa mwezi mmoja sasa wananchi wa Misri wamekuwa wakifanya maandamano katika medani maarufu ya Tahrir mjini Cairo na kulitaka Baraza Kuu la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo kutekeleza matakwa makuu ya wananchi wa nchi hiyo ambayo ni kupandishwa kizimbani na kupewa adhabu dikteta huyo wa Misri na familia yake.
Hakuna shaka kuwa kuhukumiwa Mubarak katika wakati huu ambapo Misri inapita katika kipindi muhimu, kutawafanya wananchi waliofanya mapinduzi ya kubadilisha mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo wajiamini zaidi. Matunda ya mapinduzi hayo ya wananchi wa Misri yalikuwa ni kung'olewa madarakani moja ya tawala za kidikteta za Kiarabu zilizotegemezi kwa nchi za Magharibi.
Hosni Mubarak na wanawe wawili Gamal na Alaa Mubarak, wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ambayo ni pamoja na kuua waandamanaji wakati wa harakati za mapinduzi ya wananchi wa Misri, kutumia vibaya madaraka katika miongo mitatu ya utawala wake wa kidikteta, ubadhirifu na kujilimbikizia utajiri kinyume cha sheria.
Sambamba na kusikilizwa kesi ya Mubarak, pia Habib al Adili waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Hussein Salim ambaye ni tajiri mkubwa wa nchi hiyo na dalali katika mauzo ya gesi ya Misri kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa bei ndogo zaidi kuliko ile ya masoko la kimataifa, wanatarajiwa kupandishwa kizimbani pamoja na watu wengine 6 waliokuwa maafisa wa ngazi za juu katika utawala wa zamani wa kijeshi wa Misri. Katibu mkuu wa Chama cha Kiislamu cha Amal nchini Misri amesema kuwa, kufikishwa mahakamani Hosni Mubarak na watu kadhaa waliokuwa karibu yake ni mafanikio makubwa ya mapinduzi ya tarehe 25 Januari.
Hakuna shaka kuwa kupandishwa kizimbani na mwishowe kuhukumiwa dikteta wa huyo wa zamani wa Misri ambaye kwa miongo mitatu iliyopita alilisababishia machungu makubwa taifa la nchi hiyo, kunatoa ujumbe kwamba, irada na azma ya kitaifa ina nguvu zaidi ya silaha za ukandamizaji zinazotumiwa na watawala wa kiimla dhidi ya raia katika nchi zao.

836975
captcha