Akibainisha suala hilo katika mazungumzo yake na televisheni ya al-Alam, Ahmad al-Mudallil, mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kwamba utawala wa Israel unaendesha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano wa Palestina na kwamba wanamapambano hao hawatakaa kimya mbele ya mashambulio na hujuma hiyo. Amesema viongozi wa mapambano ya Palestina wamezoea ugaidi unaotekelezwa kila siku dhidi yao na utawala ghasibu wa Israel na kwa hivyo hawataogopa vitisho vyovyote vipya vinavyotelewa na utawala huo.
Mudallil amesema makundi yote ya mapambano ya Palestina yana haki ya kujibu mashambulio ya utawala huo. Ameongeza kuwa haki hiyo inatokana na ukweli kwamba utawala huo ghasibu ndio huanzisha mashambulio na hujuma za kichokozi dhidi ya Wapalestina. Amesema kinyume na ilivyokuwa huko nyuma mapambano ya Wapalestina yameimarika sana katika miaka ya hivi karibuni, jambo ambalo limewatia Wazayuni wasiwasi mkubwa na kuwafanya sasa wawasihi Wapalestina wafanya juhudi za kutuliza hali ya mambo katika eneo hilo. 849900