Ihsanoglu amesema katika taarifa hiyo kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhani ilikuwa fursa nzuri kwa Waislamu kutakasa nafsi na roho zao. Amesema licha ya kuwa Waislamu wanasherehekea sikukuu hii muhimu ya Kiislamu kwa furaha lakini kuna wenzao ambao wanakabiliwa na matatizo pamoja na majanga mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia.
Katibu Mkuu wa OIC amesema kwa mfano nchini Libya wananchi wa nchi hiyo wanafanya juhudi kubwa za kubadilisha hali ya kisiasa ya nchi hiyo na kuirejesha katika hali ya utulivu kufuatia matukio ya hivi karibuni, ilhali nchini Somalia na nchi nyingine chache za Kiafrika Waislamu wanakabiliwa na balaa kubwa la ukame na njaa. Amewataka Waislamu katika siku hii muhimu kuwakumbuka ndugu zao wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali katika nchi hizo. Vilevile amewaomba wawasaidia kifedha na misaada mingine wanayoweza ili kupunguza machungu yao.
Pia amewataka wasaidie na kuwaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina wanaoendelea kukandamizwa na utawala ghasibu wa Israel.
Ihsanoglu amewataka Waislamu wawasaidie kwa kila njia Waislamu hao ili waweze kujibunia taifa lao huru na kuishi kwa amani katika taifa hilo. 851828