IQNA

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yalaani uvamizi dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa

13:57 - September 20, 2011
Habari ID: 2190517
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) jana Jumatatu ilitoa taarifa ikilaani vikali uvamizi uliofanywa hivi karibuni na walowezi wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa.
Katika taarifa hiyo Ekmeleddin Ihsanoglu, Katibu Mkuu wa OIC amesema kuwa uvamizi na shambulio hilo la Mayahudi wenye misimamo ya kupindukia dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa ni kuvunjiwa heshima Waislamu wote pamoja na kukiukwa sheria zote zinazohusiana na udharura wa kuheshimiwa maeneo matakatifu ya kufanyia ibada ya Mwenyezi Mungu.
Taarifa hiyo imesema kuwa watawala wa Israel ndio wanaopaswa kulaumiwa kwa shambulio hilo kwa sababu ndio wanaowaruhusu walowezi wa Kizayuni kuvunja sheria za kimataifa pamoja na Azimio la Nne la Geneva.
Ihsanoughlu ameendelea kusema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pande nne za mpango wa amani wa Mashariki ya Kati zinapaswa kutoa mashinikizo ya kutosha dhidi ya utawala huo ili usimamishe mara moja vitendo vya dharau na uvunjiwaji heshima matukufu ya kidini ya Waislamu.
Katibu Mkuu wa OIC amesisitiza kwamba vitendo hivyo bila shaka vitachochea ghasia na machafuko katika Mashariki ya Kati. Amemaliza kwa kusema kuwa OIC itaendelea kuwatetea Wapalestina wanaokandamizwa na Wazayuni hadi pale watakapopewa fursa ya kuunda nchi yao huru mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu, na kurejeshewa haki zao zote za kimsingi. 864227
captcha