IQNA

12:44 - December 01, 2011
Habari ID: 2232376

Vikwazo vya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu dhidi ya Syria ni tishio kwa mustakbali wa nchi hizo

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, amelaani vikali vikwazo vya hivi karibuni vya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu dhidi ya Syria na kusisitiza kwamba vikwazo hivyo ni tishio kubwa kwa mustakbali wa nchi hizo.

Amesema tishio hilo litatoka upande wa nchi za Magharibi ambazo zinaingilia mara kwa mara mambo ya ndani ya nchi za Kiarabu. Akifafanua zaidi suala hilo Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ambaye alikuwa kizungumza katika maombolezo ya hivi karibuni ya kukumbuka mauaji ya kinyama ya Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) huko katika eneo la Tariqul Matar mjini Beirut Lebanon, amesema kwamba kwa kutekeleza vikwazo hivyo dhidi ya Syria nchi za Kiarabu zinatekeleza vyema mpango wa Marekani wa kuvunja mapambano ya Kiislamu katika eneo.
Sheikh Naim Qassim amesema jumuiya hiyo imetekeleza mpango huo kupitia moja ya ngome muhimu za mapambano ya Kiislamu, yaani Syria. Amesema hatua hiyo ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu itakuwa na athari mbaya kwa mustakbali wa jumuiya hiyo katika siku zijazo na kupelekea kulengwa nchi zaidi zinazochukuliwa kuwa maadui wa nchi za kibeberu za Magharibi.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameelezea matumaini yake kwamba jumuiya hiyo itabadili mkondo na kujishughulisha zaidi na majukumu yake mazito na ya kimsingi ambayo ni pamoja na kutetea haki za taifa la Palestina badala ya kujishughulisha na masuala yanayozusha fitina katika ulimwengu wa Kiarabu kwa maslahi ya nchi za Magharibi.
Amesikitishwa na ukweli kwamba Jumuiya ya Nchi za Kiarabu badala ya kujishughulisha na matukufu ya nchi za Kiarabu na Kiislamu imekuwa ikiwahudumia wageni wanaotaka kudhuru nchi hizo. Amesema baadhi ya wanachama muhimu wa jumuiya hiyo wana uhusiano mkubwa na utawala haramu wa Israel ilhali wengine huogopa hata kukosoa tu siasa za utawala huo na Marekani kutokana hofu kubwa waliyonayo kuhusiana na nguvu bandia za nchi hizo, jambo ambalo amesema linailetea jumuiya hiyo aibu kubwa. 908369
captcha