IQNA

13:57 - December 24, 2011
Habari ID: 2243562

Hujuma dhidi ya misikiti yawatia wasi wasi Waislamu Ufaransa

Baraza la Waislamu wa Ufaransa limeelezea wasi wasi wake kuhusu mwenendo wa kushambuliwa misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imetoa wito kwa wakuu wa Ufaransa kuchukua hatua imara kuzuia vitendo vya hujuma dhidi ya misikiti.
Baraza la Waislamu Ufaransa limesema, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, makundi yenye chuki dhidi ya Waislamu yalitekeleza hujuma dhidi ya misikiti katika miji mbalimbali nchini humo.
Misikiti katika miji ya Roissy-En-Brie, Saint-Armant les Eaux, Montbeliard, Villeneuve-sur-Lot, Pau, na Decines ilishambuliwa katika kipindi cha kuanzia Novemba 1 hadi Disemba 20.
Hivi karibuni mtu mmoja mwenye umri wa miaka 33 alitiwa nguvuni akijaribu kuchoma moto kituo kingine cha Kiislamu. Polisi ya Ufaransa imetangaza kuwa kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi uliofanyika, mtu huyo ambaye ni mwanachama wa kundi moja la kibaguzi hadi sasa amekwishashambulia vituo saba vya ibada vya Waislamu. Polisi ya Ufaransa inafanya uchunguzi wa kutafuta wanachama wengine wa kundi la kibaguzi ambao yumkini wameshiriki katika kushambulia maeneo ya ibada ya Waislamu nchini humo.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2011 hadi sasa misikiti na maeneo 24 ya ibada na misikiti ya Waislamu imeshambuliwa na makundi ya kibaguzi katika miji mbalimbali ya Ufaransa. Polisi ya nchi hiyo inalaumiwa kwa kuzembea au kupuuza mashambulizi kama hayo yanayolenga vituo na maeneo ya ibada ya Waislamu.
920795
captcha