IQNA

Waislamu Tanzania watakiwa kuzingatia Uislamu katika malezi ya watoto

16:14 - January 11, 2012
Habari ID: 2255588
Waislamu nchini Tanzania wametakiwa kuzingatia mafundisho ya Kiislamu katika malezi ya watoto ili waweze kufanikiwa maishani.
Kwa mujibu wa tolea la Ijumaa la Jarida la Kila Wiki la Al Nur la Tanzania, msomi wa ngazi za juu wa Kiislamu nchini humo Sheikh Ali Basaleh amesema malezi bora ya watoto yanaweka msingi mzuri ambao humfanya mtoto kukua kwa kufuata maamurisho ya Allah.
Ameyasema hayo mjini Dar es Salaam wakati akihutubia semina ya walimu katika Kituo cha Kiislamu cha Markazi Chang’ombe. Maudhui kuu katika semina hiyo ilikuwa ‘Umuhimu wa Shule za Kiislamu katika Malezi ya Watoto Waislamu’.
Sheikh Basaleh amesema maadili ya watoto Waislamu nchini Tanzania yanazidi kuharibika kutokana na ukosefu wa malezi bora na mafundisho ya kumjua Allah kikamilifu. Ameongeza kuwa ili jamii iweze kujiokoa katika hali hiyo, kuna ulazima wa wazazi na walimu kufanya kazi kubwa ya kueneza maadili ya Kiislamu.
Naye kiongozi mwingine wa Kiislamu Tanzania Sheikh Suleiman Kilemile ametaka wasimamizi wa shule za Kiislamu wapewe mafunzo maalumu ili waweze kuwaongoza watoto ipasavyo. Akizungumza katika semina hiyo, Sheikh Kilemile amewataka wazazi kuwalea watoto wao katika misingi iliyo bora ili kuwasaidia walimu.
932434
captcha