IQNA

Rais wa Mauritania awataka maulamaa kupambana na misimamo ya kufurutu ada

17:31 - January 23, 2012
Habari ID: 2261551
Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania amewataka maulamaa wa Kiislamu kutoa mchango katika marekebisho ya jamii na kuonesha njia halisi ya Uislamu kwa wananchi.
Rais wa Mauritania ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa Fikra za Marekebisho na Kujiepusha na Ukatili ulioanza jana mjini Nouakchott na kuongeza kuwa katika kipindi cha sasa ambapo baadhi ya watu wenye misimamo mikali na waliojiweka mbali na mafundisho halisi ya Kiislamu wanafanya ukatili na kutumia mabavu, ni wajibu wa wanazuoni wa Kiislamu kukabiliana na watu hao na kuzuia fikra zao zisizo sahihi kwa kuarifisha Uislamu halisi.
Amesema Uislamu ni dini ya amani, utulivu na kuvumiliana, na makundi yote ya Waislamu yanapaswa kushirikiana katika kuimarisha thamani hizo katika jamii.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais wa Mauritania amesema kubainisha Uislamu halisi katika jamii ni jibu tosha kwa makundi yote yenye misimamo ya kufurutu ada ambayo yana nia ya kuarifisha Uislamu sambamba na maneno kama ugaidi, mabavu na ukatili.
Rais Ould Abdel Aziz amewataka maulamaa wa Kiislamu kushirikiana na serikali katika mapambano yake dhidi ya makundi hayo. 939649


captcha