IQNA

14:56 - February 28, 2012
Habari ID: 2282494

Wasyria wavunja njama za maadui na kuunga mkono kwa wingi mabadiliko ya katiba

Hatua ya wananchi wa Syria ya kushiriki kwa wingi katika kura ya maoni ya katiba mpya ya nchi hiyo ni ushindi mwingine kwa taifa hilo na pigo kwa maadui wake..

Weledi wa mambo amesem hatua hiyo inaweza kuondoa hali ya machafuko iliyoikumba Syria hivi sasa.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi wa Syria wanaunga mkono marekebisho ya kisiasa yanayofanywa na serikali ya nchi yao na huo ni ushindi kwa taifa hilo na viongozi wao.
Wachambuzi hao aidha wamesema, hata kama baadhi ya vyama havikushiriki kwenye kura hiyo ya maoni, lakini asilimia 57 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki na hilo linapunguza sana uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini Syria.
Huku hayo yakiripotiwa, Russia na China zimelipongeza taifa la Syria kwa kuendesha kwa amani na utulivu kura hiyo ya maoni zikisema zina matumaini kura hiyo itatatua mgogoro unaoikabili Syria.
Itakumbukuwa kuwa, jana Waziri wa Mambo ya Ndani wa Syria Bw. Muhammad ash Shaar alisema kuwa wananchi milioni 14 na laki sita wa Syria wametimiza masharti ya kupiga kura na kwamba asilimia 57 kati yao wameshiriki kwenye kura hiyo.
Zaidi ya asilimia 89 ya walioshiriki kwenye kura hiyo iliyoitishwa Jumapili Februari 26, wameipigia kura ya ndio katiba hiyo mpya.
Marekebisho hayo ya Katiba sasa yataruhusu mfumo wa vyama vingi nchini Syria. Kifungu cha 88 cha muswada huo kinasema pia kwamba mtu anaweza kuwa Rais wa Syria kwa vipindi viwili tu vya miaka saba saba na sheria hiyo itaanza kutekelezwa mwaka 2014.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa kuna sababu kadhaa ambazo zinaonesha mabadiliko hayo yanaweza kutatua sehemu kubwa sana ya mgogoro wa hivi sasa wa Syria. Wanatoa mfano wakisema, kuweko mfumo wa vyama vingi, kuwekwa uhuru mkubwa zaidi, kuwekwa kipindi maalumu cha mtu kuwa Rais na vitu kama hivyo ni miongoni mwa vipengee muhimu ambavyo kwa kiwango kikubwa vitaweza kutatua sehemu kubwa ya matatizo ya hivi sasa ya Syria.
Kwa muda sasa Rais Bashar al Assad amekuwa akifanya mabadiliko mbalimbali nchini humo. Hali ya kisiasa nchini Syria ni bora sana ikilinganishwa na nchi nyingi za Kiarabu ambazo kwa kutumia vyombo vyao vya habari vinafunika ukweli wa mambo nchini Syria na kujaribu kuonesha hakuna mabadiliko yoyote yanayofanyika nchini humo.
Nchi za Kiarabu ambazo neno demokrasia halina nafasi yoyote kwao bali wananchi wa nchi hizo wanatawaliwa na ukoo mmoja tu wa kifalme, ndizo zinazoonekana kuwa mstari wa mbele kuunga mkono magenge ya kigaidi nchini Syria kwa madai ya kupigania demokrasia. Zile nchi za Kiarabu ambazo zimepiga marufuku wananchi wake kufanya maandamano ya aina yoyote yale ili kuelezea hisia zao, ndizo hizo zinazoshirikiana na madola ya kibeberu kuishinikiza serikali ya Rais Bashar al Assad ambayo inaruhusu wananchi wa nchi hiyo kufanya maandamano kwa uhuru.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wenye chuki na taifa la Syria kutokana na misimamo ya taifa hilo ya kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina na kuwa kwake kiungo muhimu cha harakati ya muqawama hawataki kufanyike mabadiliko ya kisiasa nchini Syria msimamo ambao pia ni wa madola ya kibeberu duniani. Lakini Rais Bashar al Assad wa Syria amesema kuwa njama zote za maadui wa taifa hilo hazitamzuia kutekeleza marekebisho yote ya kisiasa kwa faida ya wananchi.
Weledi wa mambo wanaamini pia kuwa, njama za maadui wa Syria zitashindwa tu kwani wananchi wa nchi hiyo nao wako pamoja na viongozi wao katika juhudi hizo za kuleta mabadiliko ya kimsingi nchini mwao na kwa miezi kadhaa sasa miji ya Syria imekuwa ikishuhudia maandamano ya mamilioni ya watu kuunga mkono marekebisho hayo.
960519
captcha