IQNA

Misikiti inaongezeka kwa kasi Marekani

17:59 - March 03, 2012
Habari ID: 2284629
Idadi ya Misikiti nchini Marekani imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha muongo moja uliopita pamoja na kuwepo vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu baada ya matukio ya 9/11.
Kwa mujibu wa Jarida la Star Telegram, katika utafiti wa hivi karibuni imebainika kuwa kuna Vituo vya Kiislamu 2,106 kote Marekani ikilinganishwa 1,209 mwaka wa 2000 na 962 mwaka 1994.
Robo vya vituo hivyo vilijengwa kati ya mwaka 2000-2011 wakati Waislamu walikabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka vyombo vya usalama na watu wanaouchukia Uislamu. Aghalabu ya vituo vya Kiislamu Marekani hujumuisha misikiti, maktaba, shule, n.k.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2010 kuliibuka maandamano dhidi ua ujenzi wa kituo cha Kiislamu karibu na eneo la 'Ground Zero' mjini New York. Maandamano hayo yalienea katika maeneo mengine kama vile California na Tennessee.
Utafiti huu umefanywa na Profesa Ihsan Bagby wa Chuo Kikuu cha Kentucky ambaye amesema pamoja na kuwepo chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu wanazidi kujiimarisha Marekani.
Utafiti huo wenye anuani ya 'Msikiti wa Marekani 2011' imetegemea mahojiano na viongozi wa jamii za Kiislamu, uchunguzi na mahojiano na wakuu wa misikiti 424 na vile vile tovuti za intaneti.
Kwa mujibu wa utafiti huo eneo lililopewa jina la msikiti ni eneo ambalo sala ya Ijumaa husaliwa mbali na kuwepo shughuli zingine za Kiislamu. Aidha sharti jingine la jengo kutajwa kuwa ni msikiti ni kuwa lazima liwe ni milki kamili ya Waislamu. Majengo mengine yenye nafasi za kusalia sala ya Ijumaa kama vile shule na mahospitali hazikuwekwa katika orodha hiyo.
Kwa mujibu Taasisi ya Utafiti ya Pew kuna Waislamu milioni 2.75 nchini Marekani.
964416
captcha