Kwa mujibu wa tovuti ya CPI kamati hiyo ilitoa taarifa siku ya Jumamosi ikizungumzia mpango huo hatari wa utawala wa Kizayuni wa kujenga hekalu hilo karibu na Ukuta wa Buraq. Taarifa hiyo inasema kuwa tokea kutekwa Quds Tukufu na utawala wa Kizayuni mwaka 1967 hadi sasa, utawala huo umekuwa ukitetekeleza mipango mingi ya kuchimba mahandaki na njia za chini kwa chini katika eneo hilo kwa kisingizio cha kutafuta hekalu eti la Nabii Yusuf (as) hekalu ambalo halijapatikana hadi sasa. Kamati iliyotajwa ya Palestina imesisitiza kwamba ukuta wa Buraq ni sehemu isiyotenganishika ya Msikiti wa al-Aqsa, na kwamba hakuna ukuta unaojulikana kwa jina la Nudba katika eneo hilo. Inasema utawala wa Israel unatumia jina hilo kwa lengo la kupotosha ukweli wa historia ya Kiislamu. Kamati hiyo imezitaka nchi za Kiislamu na Kiarabu kufanya juhudi za kuzuia idara ya meya wa Kizayuni wa Quds kuuyahudisha mji huo, kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu, kupora nyumba na ardhi zaidi za Wapalestina pamoja na kujenga reli katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Taarifa ya kamati hiyo imesisitiza kwamba kuongezeka harakati za wananchi na kamati za mapambano, kufanyika makongamano na maandamano ya kupinga hatua hizo za utawala wa Israel bila shaka kutakuwa na athari kubwa katika kusimamisha harakati hizo za kichochezi na kichokozi za utawala wa Israel. 965350