Jumuiya ya Kiislamu ya Kielimu, Kisayansi na Kiutamaduni ISESCO imetuma ujumbe kwa nchi zote za ulimwengu wa Kiislamu kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambaye huadhimishwa Machi nane kila mwaka.
Katika ujumbe wake, ISESCO imesisitiza kuhusu ulazima wa kuhakikisha kuwa kunaandaliwa mazingira ya kuwakomboa wanawake Waislamu kutoka masaibu ya kutojua kusoma na kuandika, ujinga na mila potofu zinazokiuka mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume SAW.
ISESCO pia imesisitiza kuhusu ushiriki wa wanawake katika masuala ya umma kwa lengo la kuimarisha hali yao ya kimaisha na kusema hilo ni jukumu la kidini. ISESCO imetoa wito kwa viongozi wanawake katika serikali, taasisi, jumuiya na mabunge kufanya juhudi za kuimarisha masuala ya wanawake ili kuhakikisha kuwa wanapata nafasi na hadhi wanayostahiki kama ilivyoainishwa katika mafundisho ya Kiislamu.
Katika taarifa hiyo shirika la ISESCO limesema litajitahidi kustawisha shughuli na program za kuboresha maisha ya wanawake katika ulimwengu wa Kiislamu.
966354