Taarifa hiyo imesema jinai hiyo kubwa inabainisha chuki kubwa na ya muda mrefu aliyo nayo kasisi huyo wa Marekani. Hizbullah imesema katika taarifa hiyo kwamba Terry Jones amechukua hatua hiyo ya kipumbavu kwa lengo la kueneza chuki na uadui dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi. Imesema katika hatua yake ya kwanza ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu watu huenda walidhani kwamba hatua hiyo ilitekelezwa bila kuwepo mipango maalumu, lakini kwamba kukaririwa kitendo hicho na kasisi yuleyule aliyekitekeleza mara ya kwanza huku watawala wa Marekani wakiwa wamekaa kimya, ni jambo linalothibitisha kwamba kitendo hicho kinafanyika kwa makusudi na kwa uungaji mkono wa White House.
Taarifa ya Hizbullah imeendelea kusisitiza kwamba kufanyika kitendo hicho wakati unaokaribiana na ule wa kuchomwa moto nakala za Qur'ani na askari wa Marekani huko Afghanistan ni jambo linalotilia nguvu ukweli huo.
Hizbullah inasema kwamba watawala wa Marekani wanapasa kubebea moja kwa moja lawama za kuchomwa moto kitabu hicho kitakatifu kwa sababu hawakuchukua hatua za lazima za kumzuia kasisi huyo mwovu kutekeleza tishio la kukichoma moto wala kulaani kitendo hicho.
Harakati hiyo ya Kiislamu ya Lebanon imezitaka nchi zote za Kiarabu na Kiislamu na wale wote wanaotetea thamani za kidini kuchukua msimamo mkali dhidi ya watu wanaovunjia heshima matukufu ya kidini. 998200