IQNA

Mashia wa Nigeria washerehekea uzawa wa Bibi Fatma (as)

18:28 - May 15, 2012
Habari ID: 2326725
Waislamu wa eneo la mji wa Zaria nchini Nigeria wamesherehekea uzawa wa Bibi Fatma az-Zahra (as) binti ya Mtume Mtukufu (saw) kwa muda wa siku tatu mfululizo.
Sherehe hizo zimefanyika katika Husseiniya ya Baqiyatullah iliyoko mjini humo. Sherehe hizo za kufana zilifanyika tokea siku ya Jumamosi hadi Jumatatu tarehe 14 Machi. Katika sherehe hizo wafuasi na wapenzi wa wa Ahlul Beit (as) yaani Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) walikusanyika na kunufaika na hotuba za shakhsia tofauti wa Kiislamu waliozungumza katika sherehe hizo akiwemo Sheikh Ibrahim Yaaqub Zakzaki, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye aliwasihi Waislamu na watu wote kuzingatia kwa kina nafasi ya mama na mwanamke katika jamii. Ameashiria maisha ya ndoa ya Bibi Fatma na Imam Ali (as) na jinsi watukufu wawili hao walivyoamiliana kwa heshima na kuzingatia uchaji Mungu na kusisitiza kuwa shakhsia wawili hao wanaweza kuchukuliwa kuwa mfano bora zaidi wa ndoa zilizofanikiwa na za kuigwa duniani. Ameongeza kwamba Waislamu kote duniani wanapasa kuwaiga watukufu wawili hao kama mfano bora zaidi wa maisha ya mume na mke na uchaji-Mungu katika maisha yao ya kila siku. Amesema wanaume wanapasa kuheshimu na kuamiliana vyema na wake zao maishani. 1007666
captcha