Sherehe ya uzinduzi wa ujenzi wa msikiti huo ambao umepewa jina la Msikiti Mkuu wa Algiers ilihudhuriwa na Bu Abdallah Ghulamullah, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kidini wa Algeria pamoja na Liu Yuhi Balozi wa China nchini Algeria. Msikiti huo unajengwa katika mtaa wa Muhammadiya mashariki mwa mji mkuu huo. Mkataba wa ujenzi wa msikiti huo ulitiwa saini mwezi Machi mwaka uliopita kati ya shirika la China la CSCEC na Shirika la Kitaifa la idara ya Msikiti Mkuu wa Algeria. Kwa mujibu wa mkataba huo wafanyakazi za mikono wapatao 17,000 watashiriki katika ujenzi wa msikiti huo ambapo 10,000 watakuwa ni raia wa Algeria. Msikiti huo ambao utakuwa na uwezo wa kubeba watu 120,000 utakuwa wa tatu kwa ukubwa duniani baada ya misikiti ya Masjidul Haram na Masjidu Nabi (saw). Mbali na msikiti huo Darul Qur'an al-Karim, Kituo cha Utamaduni wa Kiislamu, vibanda vya maonyesho ya kudumu, maktaba, ukumbi wa mikutano, jumba la maonyesha ya mambo ya kale ya Kiislamu na kituo cha utafiti pia vitajengwa katika uwanja wa msikiti huo. 1013383