Wakizungumza siku ya Jumapili huko Moscow, mji mkuu wa Russia, katika kongamano la kimataifa la 'Mafundisho ya Kiislamu katika Kupambana na Misimamo ya Kupindukia Mipaka,' wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu wamekosoa na kulaani utumiaji mabavu na fikra za kupindukia mipaka kidini ulimwenguni.
Kongamano hilo lililoandaliwa kwa lengo la kulaani fikra za kupindukia mipaka zinazodhihirishwa na baadhi ya makundi ya kidini limefanyika kwa udhamini na ushirikiano wa Muungano wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Russia, Kituo cha Utafiti na Mafunzo cha nchi hiyo pamoja na Kituo cha Kimataifa cha al-Wasatiya cha Kuwait. Kutafuta njia za kutumiwa maneno mbadala badala ya maneneo yaliyozoeleka ya Kiislamu kama vile 'jihadi', 'ukafiri' na 'ukhalifa' ni miongoni mwa masuala muhimu yaliyochunguzwa katika kongamano hilo. Washiriki wa kikao hicho wanasema kuwa utumizi mbaya wa maneno hayo katika zama hizi kumechochea vitendo vya mabavu na chuki dhidi ya Waislamu nchini Russia na nchi nyingine za dunia. Kwa mujibu wa Baraza la Mamufti wa Russia kongamano hilo la siku mbili limewashirikisha wanazuoni, wasomi na wanafikra wa Kiislamu kutoka nchini humo na katika nchi nyingine za kigeni zikiwemo za Kuwait, Lebanon, Morocco, Bahrain, Syria na Tunisia. 1018733