IQNA

Imam Khamenei awataka wabunge Iran kuwa na ikhlasi, kutawakali kwa Allah

14:40 - June 14, 2012
Habari ID: 2346617
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano ameonana na wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kusema kuwa, bunge linapaswa kuwa na sifa zote za kulifanya kuwa bunge hai katika kazi zake na katika kutekeleza majukumu yake muhimu na ya kimsingi kama ambavyo linapaswa pia kuwa Bunge salama lenye nishati ya hali ya juu katika vipengee mbali mbali vya kisiasa, kimaadili na kifedha.
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumatano) ameonana na wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kusema kuwa, bunge linapaswa kuwa na sifa zote za kulifanya kuwa bunge hai katika kazi zake na katika kutekeleza majukumu yake muhimu na ya kimsingi kama ambavyo linapaswa pia kuwa Bunge salama lenye nishati ya hali ya juu katika vipengee mbali mbali vya kisiasa, kimaadili na kifedha.
Aidha amelitaja suala la kuwa na hisia za kutekeleza vizuri majukumu, kuwa na nia ya ikhlasi, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutochoka katika jitihada za kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kuwa ni mambo yanayoandaa mazingira ya kupatikana ufanisi katika kazi za bunge na taasisi nyingine nchini na kuongeza kuwa, kama mtazamo na moyo huo utatawala, basi kwa baraka, rehema na msaada wa Mwenyezi Mungu, njia nyingine nazo zitafunguka na matatizo yote yatatatuliwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kutegemea uwezo usio na mwisho wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo siri ya kuwa na nguvu na kupiga hatua za maendeleo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, mfumo wa Kiislamu nchini Iran, umesimama imara kulinda matukufu ya Mwenyezi Mungu na ya kibinaadamu katika dunia hii iliyogubikwa na masuala ya kimaada na kwamba wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wanapaswa kulitambua vilivyo na kwa kina jambo hili kwamba, kuwa na uhusiano mzuri na Mwenyezi Mungu ndiyo siri ya kweli ya kupata mafanikio (duniani na Akhera).
Aidha amesema uadui wa mabeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na dhati ya waistikbari hao ya kupenda kuyadhulumu na kuyafanyia ubeberu mataifa mengine na kuongeza kuwa, baadhi ya watu wanatumia mafumbo na kudai kuwa msiifanye dunia ilazimike kukabiliana na utawala wa Kiislamu nchini, lakini anayesema maneno hayo huwa hakuchunguza asili ya mambo kwani suala la kuundwa serikali ya kidini na demokrasia ya kidini, lenyewe kwa udhati wake lina maana ya kukabiliana na mafirauni wa dunia na hilo ndilo lililowafanya mabeberu hao wa dunia kukabiliana na mfumo huu wa utawala na taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema, bunge ni nguzo muhimu sana ya utawala wa Kiislamu nchini Iran na amebainisha sifa mbili muhimu inazopasa kuwa nazo Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani kuwa hai na salama na kuongeza kuwa, bunge lisilo na harakati, lililotulia tuli na linalopitisha mambo yasiyo sawa, ni bunge pungufu na kwamba watu waliochaguliwa na wananchi wanapaswa kuhakikisha kuwa bunge linakuwa na sifa yake inayotakiwa, yaani nishati na harakati.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kutekeleza majukumu ya kimsingi ya bunge yaani kutunga sheria nzuri na kusimamia kwa njia sahihi masuala iliyopewa kuyasimamia ni ushahidi wa wazi wa kuwa na bunge hai na kuongeza kwamba, wabunge wa Majlisi ya Tisa ya Ushauri ya Kiislamu wanapaswa kufanya kazi zao chini ya misingi na vielelezo vya sheria nzuri na usimamiaji sahihi.
Ameongeza kuwa, usimamiaji unaotokana na nia mbaya, usimamiaji wenye upendeleo na usimamiaji ambao hauangalii mambo kwa kina ni miongoni mwa usimamiaji mbaya sana usio sahihi hata kidogo na kusisitiza kwamba, kama mambo yatafanyika hivyo, basi itakuwa ni ushahidi wa wazi kuwa bunge halina sifa yake inayostahiki kuwa nayo.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amekutaja kuhudhuria kushiriki vilivyo na kwenye faida katika vikao vya wazi vya bunge na katika kamisheni mbali mbali za bunge kuwa ni mambo mengine yanayoonyesha kuweko hai Bunge hilo na kuongeza kwamba, kutoshiriki na kuthohudhuria inavyoopasa katika vikao vya bunge na kutochangia mijadala bungeni na katika kamisheni zake ni miongoni mwa matatizo ambayo Bunge la Tisa la Iran linapaswa kujiepusha nalo kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kujitokeza vilivyo katika masuala ya kisiasa ya ndani ya nchi na ya kieneo na kimataifa kuwa ni jambo jengine la dharura kwa bunge lililo hai na lenye nishati na harakati nyingi na kuongeza kuwa, bunge ni dhihirisho la wazi la "mapinduzi, fikra za watu wote na siasa kuu" za nchi na kwamba inabidi bunge liwe na misimamo yake maalumu na ya wazi kuhusu matukio na masuala ya ndani na nje ya ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matukio na mabadiliko makubwa na yenye kasi kubwa yanayoshuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa, hivi sasa kuna makelele mengi katika eneo hili. Pia amesema, eneo hili muhimu ambalo linahesabiwa kuwa ni kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu, hivi sasa linatawaliwa na hali ya ajabu.
Amebainisha kuwa: Kama wabunge watachukua misimamo mizuri na kwa wakati unaofaa kuhusu matukio yanayojiri kwenye eneo hili, basi bila ya shaka jambo hilo litatoa taathira pia kwa wananchi wa mataifa ya eneo hili na kwa nchi zenye ushawishi na zinazohusika katika matukio ya eneo hili zima.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kubainisha sifa ya pili na ya dharura inayopasa kuwa nayo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani kuwa kwake salama akisema kwamba, hatua ya bunge na kila mjumbe katika bunge hilo ya kuwa salama katika masuala ya kisiasa, kimaadili na kifedha ni jambo la dharura kabisa.
Ameongeza kuwa, kama kutatokezea mrengo japo mdogo ukawa unapinga baadhi ya misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu bungeni, ijulikane kuwa huko ni kukosekana usalama wa kisiasa katika bunge.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, kutojali kilio ambacho ni wajibu kusikilizwa na kuhisi majukumu juu yake na vile vile kutoshughulishwa na masuala ya matumizi ya fedha ni ishara nyingine za kutokuwa salama bunge na kusisitiza kwamba: Bodi ya Uongozi ya Bunge na wabunge wote wengine wanapaswa kufanya juhudi zao zote kuhakikisha kuwa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linakuwa kigezo kizuri katika kupunguza gharama za matumizi.
Amesisitiza kwa kusema: Tab'an miongoni mwa wawakilishi wa bunge, kuna watu wengi tu ambao wanachukua tahadhari kubwa na kuchunga sana mambo yao na huu ni uhakika muhimu na unaostahiki kusifiwa na kushukuriwa.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameashiria tahadhari alizotoa miaka kadhaa nyuma juu ya umuhimu wa wabunge kujisimamia na kujichunguza wenyewe na kuongeza kwamba: Tab'an kuna hata sheria imepitishwa kuhusu suala hilo na kuna ulazima wabunge wenyewe wajisimamie na wajichunge na kujitathmini wao wenyewe na wabunge wenzao wakati wote ili kulilinda bunge na kulifanya liwe salama.
Kujiepusha kuwavunjia heshima watu wengine ni jambo jengine ambalo limeashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kama dalili muhimu ya kuwa salama bunge.
Vile vile amewasisitizia wabunge hao waliochaguliwa na wananchi akisema: Mnapozungumza tambueni kuwa mnazungumza mbele ya spika ya taifa hivyo mnapaswa mchukue tahadhari sana msije mkawavunjia watu wengine heshima wala kutoa tuhuma zisizo na uthibitisho na wala kuingilia masuala binafsi ya watu.
Kupiga makelele na kuzusha mabishano yasiyo na maana baadhi ya wabunge wakati wa kuzungumza wabunge wenzao au viongozi wa serikali ni kitu kingine kilichokosolewa vikali na Ayatullah Udhma Khamenei katika hotuba yake ya leo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Bungeni ni sehemu pa kufanyika mazungumzo na mijadala kwa njia za busara na hekima na jambo hilo linakinzana kikamilifu na suala la kupiga makelele wakati watu wengine wanazungumza na kwamba tabia hiyo mbaya sana na ya kushangaza inabidi iondolewe kikamilifu katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa huru bunge kuwa ni suala muhimu mno na ni katika dalili za kuwa salama bunge. Amesema pia kuwa ametoa nasaha hizo kwa serikali zote zilizopita na kwa vipindi vyote vilivyotangulia vya bunge kwamba si sahihi kwa bunge kupinga kila kitu cha serikali kwa sababu tu ya kutaka bunge liwe huru.
Aidha ikumbukwe pia kwamba, kama bunge linapinga kitu fulani, basi linaweza kutunga sheria kuhusu jambo hilo na sio kuchukua hatua zisizo za kimantiki.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amelitaja suala la umoja na mshikamano kuwa ni jambo muhimu na la dharura sana hivi sasa na kuongeza kwamba, suala la kuwa na mshikamano na kuwa kitu kimoja kifikra, halikinzani hata kidogo na mtu kutoa fikra na mitazamo inayotofautiana na wenzake, lililo muhimu ni kwamba wakati watu wanapotofautiana kifikra na kimitazamo, kutofautiana kwao kusiwe sababu ya kugombana na inabidi mikono ya viongozi wote nchini iwe imeshikamana na kuwa kitu kimoja wakati wote, na kila mtu afanye juhudi za kuinyanyua juu nchi na kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwa na hitilafu na ugomvi kuwa ni dalili za udhaifu na kuongeza kuwa, kumeainishwa marejeo maalumu ya kuweza kurejea kwake wakati zinapotokea tofauti za mitazamo na kwamba sheria na mtazamo wa Baraza la Kulinda Katiba ndivyo vitu vinavyoweza kubainisha vizuri zaidi (aliye na haki wakati wa zinapozuka tofauti kama hizo) na katika hali yoyote itakayoamuliwa, jukumu la kila mmoja na kila kiongozi nchini ni kulinda umoja na mshikamano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kwa kusema: Tab'an pande zote mbili au tatu zinazotofautiana katika jambo fulani zote zinakubali kuwa si jambo zuri kuwa na hitilafu, lakini katika matendo utaona kunashuhudi baadhi ya hitilafu zikijitokeza hata ndani ya baadhi ya taasisi na vyombo vyenyewe vinavyotofautiana kimitizamo na vyombo vingine, hivyo inabidi kuwa macho na kulinda umoja na mshikamano wakati wote.
Aidha amemshukuru Dk. Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran kwa hotuba yake nzuri na yenye faida kubwa aliyoitoa kwenye mkutano huo na kusema kuwa: Tuna matumaini makubwa kwamba bunge litaendelea kuwa huru, litakuwa na fikra za kujitegemea, litaendelea kulinda maslahi ya nchi, litazidi kuwa shujaa mbele ya adui na litapangilia vizuri kazi zake likiwa na matumaini mazuri kuhusu mustakbali bora wa taifa hili.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mustakbali bora wa unaong'ara wa taifa la Iran na wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni uhakika uliobashiriwa tangu zamani na pia amelishukuru taifa la Iran kutokana na imani yake ya kidini na vijana wake wazuri na kuongeza kuwa, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mhimili wa harakati kuu ya nchi utaendelea kuwa ni tafakuri na kushikamana na mafundisho ya kidini na Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea matumaini yake akisema: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, muongo huu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao unajulikana kwa jina la muongo wa maendeleo na uadilifu nchini, Iran itaweza kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo na mwishoni mwa muongo huu, kiwango cha uadilifu kitapanda mno humu nchini.
Mwanzoni mwa mkutano huo na kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk. Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amegusia vipindi mbalimbali vya mabaraza ya utungaji sheria nchini Iran na kuvitaja vipindi vya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni vipindi bora kabisa vya bunge nchini Iran. Ameongeza kuwa: Katika kipindi hicho cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, bunge la Iran limetunga na kupasisha sheria nyingi na kupiga hatua kubwa za kuiletea maendeleo nchi kwa kutegemea misingi ya uhuru na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Vile vile ametilia mkazo udharura wa kutungwa ramani ya njia kwa ajili ya kudhamini manufaa ya taifa na kuandaa uwanja wa kupatikana utulivu mkubwa na usio na doa nchini. Pia amekutaja, kufuatilia kwa karibu na kwa kuendelea matukio mbali mbali nchini na kulinda haki za taifa la Iran kuwa ni miongoni mwa majukumu makubwa ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Vile vile Spika wa Bunge la Iran ametoa ripoti kuhusu idadi na aina ya wabunge wapya waliochaguliwa kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na kusema kuwa, kushikamana na malengo matukufu ya mapinduzi ya Kiislamu na kuwa na ushujaa mkubwa katika kulinda haki za taifa la Iran ni miongoni mwa sifa maalumu zinazoonekana wazi wazi za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran.

1029355
captcha