IQNA

Fadhila za kiakhlaki za Bibi Fatma (as) zabainishwa katika semina ya Uturuki

16:35 - June 17, 2012
Habari ID: 2348810
Fadhila za kiakhlaqi za Bibi Fatma (as) binti wa Mtume Mtukufu (saw) zimejadiliwa katika semina iliyoandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Kiutamaduni na Mafunzo ya nchini Uturuki.
Katika semina hiyo iliyofanyika Jumatano iliyopita wanaharakati wa kike wa Uturuki wamewataka wanawake wa nchi hiyo kufuata mfano bora kiakhlaqi na kimaadili wa Bibi huyo mtukufu wa Kiislamu (as).
Akizungumza katika semina hiyo, Hatun Pulad mkuu wa jumuiya iliyotajwa amesema kuna haja kubwa kwa wanawake na mabinti wa kizazi kipya kufuata maishani mfano bora wa Bibi Fatma (as) ambaye alipata mafunzo mema ya Mtukufu huyo (saw). Amesema watu wanaojaribu kuhadaa wanawake na kutumia vibaya nafasi yao katika jamii kwa kisingizio cha uhuru na demokrasia wanapasa kutambua kwamba wanawake wa Kiislamu hawatahadaika na uongo huo bali wataendelea kushikilia misimamo yao ya kuthamini thamani na mafundisho matukufu ya Kiislamu. Amesema wanawake wa Kiislamu wa Uturuki wataendelea kuheshimu na kuiga fadhila za watukufu wa kidini na hasa Bibi Fatma (as).
Halima Achiqkuz, mzungumzaji mwingine katika semina hiyo amesema nchi za Magharibi zimekuwa zikifanya juhudi za kueneza utamaduni mchafu wa uchi katika nchi za Kiislamu lakini akasisitiza kuwa Waislamu na hasa wanawake wanapasa kuendelea kushikilia utamaduni wao uliosimama juu ya msingi na mafundisho ya Kiislamu.
Amesema wanambua vyema hali mbaya aliyokuwa nayo mwanamke kabla ya kudhihiri Uislamu na kwamba dini hii tukufu ndiyo iliyomrejeshea mwanamke hadhi na thamani kubwa na hivyo wanapasa kuilinda kwa kila njia. 1031125
captcha