IQNA

Sahifa Sajjadiya ya Imam Zainul Abidin AS

11:58 - June 25, 2012
Habari ID: 2353911
Tuko katika siku adhimu na zilizojaa baraka za mwezi wa Shaaban. Siku ya tano ya mwezi huu inasadifiana na uzawa wa ‘Ali ibn Al-Hussein AS ambaye anajulikana kama Zayn al-‘Ābidīn au mbora wa wanaoabudu.
Aidha ni maarufu kama Sayyid as-Sājjadīna wa r-Rāki‘īn yaani bwana wa wanaosujudu na kurukuu na hivyo lakabu yake mashuhuri ni Sajjad. Yeye ni Imam wa nne katika kizazi cha Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW.
Imam Sajjad AS ni shakhsia mkubwa ambaye alichukua jukumu la Uimamu na uongozi wa umma katika kipindi muhimu sana cha historia ya Uislamu yaani baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hussein AS.
Mtukufu huyo, katika maisha yake yaliyojaa baraka na katika kipindi cha miaka 34 ya Uimamu wake, aliacha kumbukumbu ya mafundisho yaliyojaa thamani. Sehemu ya mafunzo haya ni kitabu chake chenye thamani chungu nzima kinachojulikana kama Sahifa Sajjadiya. Kwa hakika Sahifa Sajjadiya ni moja ya johari au hazina zenye thamani, iliyokusanya maarifa ya Mwenyezi Mungu ndani yake. Mjumuiko huu uliojaa nuru ingawa uko katika muundo wa dua kwa Mola muumba lakini pia ni mfumo kamili wa malezi.
Imam Sajjad AS alitoa darsa za hali ya juu zaidi za kiitikadi, kiakhlaqi na kijamii kwa kutumia lugha ya dua. Yaliyomo katika Sahifa Sajaddiya ni masuala ambayo mwanaadamu anayahitaji katika kila zama na wakati.
Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Imam Sajjad AS na kuwakaribisha kusikiliza machache tuliyowaandalia kuhusu mfumo wa malezi wa Imam Sajjad AS katika Sahifa Sajaddiya.
Mwanaadamu ana kipaji cha kufikia kwenye ubora wa kiroho na kimaanawi. Lakini kufikia ubora huu kunawezekana tu kupitia malezi sahihi. Kwa yakini njia bora zaidi ya malezi inaweza kupatikana katika maneno na sira za wanaadamu waliokamilika katika kila zama. Hawa ni wanaadamu ambao ni vigezo vya maisha katika zama zote. Kwa kuangazia sira na maneno ya Mtume Muhammad SAW na Ahul Bayt wa mtukufu huyo AS, tunafahamu kuwa maarifa ya watukufu hao yamebainisha ramani iliyokamilika ya maisha yaliyojaa heshima na saada.
Imam Sajjad AS alisisitiza kuwalea wanaadamu katika mhimili wa tauhidi na kwa hivyo alitilia mkazo ufahamu wa kina wa masuala kama vile kumuabudu Mola muumba, maarifa ya Mwenyezi Mungu, imani na takwa.
Katika kitabu cha dua cha Sahifa Sajjadiya, Imam Sajjad AS anaarifisha lengo lake kuwa ni kuwalea wanaadamu ili kupata ridhaa ya Allah SWT na kujikurubisha kwa Mola wake. Katika kitabu hicho, kwa kutumia lugha ya dua, Imam Sajjad AS anawaongoza waja kuelekea katika uhakika wa tauhidi. Lugha ya dua iliyotumika katika Sahifa Sajjadiya kwa lengo la kuelimisha na kulea ni lugha ya mhemuko, akili, mantiki, upendo na maarifa na hivyo kuitayarisha roho ya mwanaadamu kupokea ukweli.
Katika dua zake mbali mbali, Imam Sajjad AS anatufunza kuwa Allah SWT anapaswa kuwa mhimili wa maisha ya mwanaadamu katika vipindi vyote vya maisha yake. Anasema lengo la kumfanya Allah SWT awe mhimili ni kuwezesha maisha yetu yatawaliwe na Allah SWT. Mfungamano wa mwanaadamu na Mwenyezi Mungu katika Sahifa Sajjadiya unaanzia katika maarifa na kumjua Mwenyezi Mungu.
Moja ya sifa pekee za mfumo wa malezi katika Sahifa Sajjadiya ni kuambatana kwake na fitra ya mwanaadamu.
Imam Sajjad AS kwa kufahamu kikamilifu mahitajio ya kifitra ya mwanaadamu, aliyatumia mahotajio hayo katika malezi. Moja ya mahitajio ya kifitra ya mwanaadmu ni kumtafuta Mwenyezi Mungu na kuzingatia dhati ya haki. Imam alitumia hitajio hili kama mazingira ya kubainisha masuala ya ibada na ucha Mungu na hivyo kuitayarisha roho kupokea neema ya Mwenyezi Mungu.
Imam Sajjad AS alitumia sentensi maridadi sana na zenye kutuliza moyo katika kumsifu na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu ni moja ya malengo ya juu kabisa katika maisha ya humu duniani. Suala hili lina umuhimu mkubwa sana na Imam Sajjad AS amelitaja kuwa sababu ya mtu kupata utulivu. Katika Dua ya 47 ya Sahifa Sajjadiya tunasoma hivi: “Ewe Mola! Nipe makao ya kupumzikia yatakayonipa utulivu na yawe sehemu ya kupumzishia macho yangu.”
Makao haya ya kupumzikia yatakuwa yaliyojaa furaha pale mwanaadamu atakapotumia vitu vyake vyote duniani kama njia ya kujikuribisha kwa Mwenyezi Mungu. Katika dua ya 30 ya Sahifa Sajjadiya tunasoma hivi: “Ewe Mola! Ifanye mali na vitu vya dunia ulivyonipa viwe njia ya kukufikia wewe na njia ya kunifikisha peponi.”
Kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kuna maana ya kufanya kila kitu kwa ajili yake na mkabala wa hilo ni kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu.
Imam Sajjad AS katika dua ya 20 ya Sahifa Sajjadiya anamuomba Mwenyezi Mungu hivi: “Ewe Mola! Nijaalie nije kwako wakati wa matatizo na niombe msaada wako kwa ninayohitajia na wala nisishawishike kuomba msaada kwa yeyote isipokuwa wewe…..”
Dua hii inasisitiza kuwa mwanaadamu kwa dhati yake huelekea kwa Mola wake wakati akiwa na matatizo na akiwa ni mhitaji.
Imam Sajjad AS pia katika dua zake, mbali na masuala ya malezi pia anazingatia masuala ya neema za Mwenyezi Mungu. Anakumbusha kuhusu neema za Mwenyezi Mungu ambazo mwanaadamu huwa ameghafilika nazo kutokana na kujishughulisha na maisha ya kidunia.
Katika mfumo wa malezi wa Imam Sajjad AS, kukumbuka neema kunapaswa kuwa katika fremu ya kumhimidi na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, katika dua ya kwanza ya Sahifa Sajjadiya, Imam Sajjad AS anakumbusha kuhusu neema kwa kumhimdi Mwenyezi Mungu na kisha kusisitiza kuhusu kutubu mja na kurejea kwa Mola wake.
Mtukufu huyo katika dua hiyo anamsifu Mwenyezi Mungu kwa kuweka wazi mlango wa toba kwa wanaadamu. Anamtaja mwanaadamu aliyefikia ubora na ufanisi kuwa ni yule ambaye anarejea kwa Mola wake. Toba katika Sahifa Sajjadiya imetajwa kuwa msingi muhimu katika malezi ya mwanaadamu. Kwa mtazamo wa Imam Sajjad AS, toba kwa maana yake halisi haihusiani tu na madhambi na maasi bali kujiweka mbali na lile duara la kumridhisha Mwenyezi Mungu ni jambo linalohitajia toba.
Imam Sajjad AS anampa mwanaadamu matumaini kuhusu rehema na maghfira ya Allah SWT na kulitaja suala la matumaini kuwa msingi mwingine muhimu katika malezi ya mwanaadamu. Kutumia mbinu hii humpelekea mwanaadamu kuingia katika medani ya amali kwa roho tulivu na yenye yakini na hivyo kuleta mabadiliko katika mwendo wake. Katika sehehmu ya dua ya 12 ya Sahifa Sajjadiya tunasoma hivi: “Ewe Allah! Unastahiki sifa zote, sipotezi matumaini kwako kwani umeniwekea wazi mlango wa toba.”
Halikadhalika katika sehemu ya Dua ya 16 ya Sahifa Sajjadiya, Imam Sajjad anabainisha anavyostaajabu kuhusu namna Mwenyezi Mungu anavyoamiliana kwa ukarimu na waje wake.
Kiujumla ni kuwa katika Sahifa Sajjadiya, Imam Sajjad AS anamuonyesha mja namna ya kunong’ona na Mola wake na kumuomba neema, uwezo, afya, maadili bora, rizki pana na vile vile kuomba kuondolewa balaa, maradhi n.k. Katika dua zake, Imam Sajjad AS ameomba vitu vya kimaada ili kwa kujibiwa dua yake, katika kivuli cha ibada na ucha Mungu, mwanaadamu aweze kuandaa mazingira ya kupata roho iliyokamilika na ya kimaanawi.
Katika sehemu nyingine ya Sahifa Sajjadiya, suala la uhusiano baina ya wanaadamu limezingatiwa ambapo tunaona mitazamo maalumu kuhusu malezi imepewa uzito. Kimsingi ni kuwa mfumo wa malezi katika Sahifa Sajjadiya unalenga kumjenga mwanaadamu katika sekta mbali mbali za maisha ya kifamilia, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa mfano tunaona katika Sahifa Sajjadiya suala la uhusiano wa mtoto na mzazi limezingatiwa. Katika dua ya 24 ya Sahifa Sajjadiya tunaona dua ya Imam Sajjad AS akizungumzia wazazi wake na hapo inabainika wazi nafasi ya juu ya mama na baba na wadhifa wa watoto.
Tunachukua fursa hii kuwausia mkisome kitabu cha Sahifa Sajjadiya ambacho kimetarujumiwa kwa lugha kadhaa zikiwemo za Kiingereza na Kiswahili. Tunawaaga kwa sehemu hii ya dua ya Imam Sajjad AS kuhusu wazazi aliposema: “Ewe Mola! Ijaalie sauti yangu iwe ya chini mbele yao, yafanye maneno yangu yawe ni yenye kukubalika mbele yao, ihafifishe hasira yangu mbele yao, ifanye roho yangu iwe laini mbele yao na nijaalie niwe mshirika wao mkarimu….”

1037582
captcha