IQNA

17:44 - July 01, 2012
Habari ID: 2358069

Rais Mursi wa Misri: ‘Tutasimama pamoja na watu wa Palestina’

Rais Mohammad Mursi wa Misri amesema nchi yake itasimama bega kwa bega na Wapalestina hadi wapate haki zao.

Akihutubu katika Chuo Kikuu cha Cairo baada ya kuapishwa, Mursi amesema serikali na watu wa Misri wako pamoja na Wapalestina ambao wanadhulumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mursi pia ametoa wito wa kusitishwa umwagaji damu nchini Syria.
Mapema jana Mursi alikula kiapo cha urais mbele ya Mahakama Kuu ya Katiba ya nchi hiyo.
Katika sherehe hizo Mursi aliapa kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu kwamba, atalilinda taifa, kuheshimu katiba, sheria za nchi yake sambamba na kulinda maslahi ya taifa la Misri.
Utawala ghasibu wa Israel umekumbwa na wasiwasi mkubwa kufuatia ushindi wa harakati ya Ikhwanul Muslimina nchini Misri. Utawala huo ulibainisha wasiwasi huo baada ya kutangazwa ushindi wa Muhammad Mursi na kuongeza kuwa, ushindi huo utaharibu uhusiano uliokuwepo kati ya Israel na Misri.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, wasiwasi huo unatokana na kuwepo uwezekano wa kuvunjika mkataba wa Camp David uliotiwa saini mwaka 1978 na watawala wa zamani wa nchi hizo.
Nayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imetoa pongezi kwa wananchi wa Misri kufuatia ushindi huo na kuongeza kuwa, ushindi wa Muhammad Mursi ni tukio muhimu katika historia ya taifa la Misri na kuhitimishwa ushirikiano wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni.
Hayo yalisema hapo jana na msemaji wa harakati hiyo Sami Abu Zuhri na kuongeza kuwa, ushindi huo umewafurahisha pia wananchi wa Wapalestina hususan wakazi wa Ukanda wa Gaza ambao wamekuwa katika mzingiro wa muda mrefu unaotekelezwa na utawala wa Kizayuni.
1041786
captcha