IQNA

Ufaransa yakaidi amri ya FIFA ya kuruhusu vazi la Hijab

11:51 - July 08, 2012
Habari ID: 2363159
Shirikisho la Soka Ufaransa limetangaza kuwa halitaruhusu wanawake Waislamu wachezao soka kuvaa hijabu, hatua amabyo ni ukiukwaji wa wazi wa amri ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA iliyoamuru kuwa wanawake waruhusiwe kuvaa hijabu katika michezo ya kimataifa.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Shirikisho la Soka Ufaransa limetoa taarifa katika tovuti yake rasmi na kusema 'hatutaruhusu wachezaji wanawake kuvaa hijabu.'
Hivi karibuni FIFA ilibatilisha uamuzi wake wa mwaka 2007 wa kupiga marufuku vazi la hijabu ya Kiislamu.
Katika kuondoa marufuku hiyo Michel D'Hooghe Mkuu wa Kamati ya Afya ya FIFA alisema, ‘matatizo niliyokuwa nayo kuhusu vazi la Hijabu yalikuwa ya usalama wa kiafya na sasa sina mushkili na suala hilo tena.’
Mwezi Machi mwaka 2012 Bodi ya Kimataifa ya Soka IFAB iliwaruhusu wanawake waislamu kuvaa vazi la hijabu.
Aprili mwaka huu FIFA ilitangaza kuwa itapiga marufuku uvaaji hijabu katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012 mjini London.
Mwaka jana Timu ya Soka ya Wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizuiwa kushiriki katika raundi ya pili ya kuwania tiketi ya michezo ya Olimpiki dhidi ya Jordan baada ya kukataa kuvua vazi la Kiislamu la hijabu zao.
Iran ambayo ilikuwa inaongoza kundi hilo ilikoseshwa fursa ya kushiriki katika michezo ya Olimpiki huko London kutokana na marufuku hiyo.
Hatua ya Ufaransa kukataa wanawake Waislamu wavae hijabu wanapocheza soka ni katika fremu za sera za chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya Ulaya. Tayari vazi la hijabu imeshapigwa marufuku katika taasisi kadhaa za umma nchini humo.
1047364
captcha