IQNA

Uchaguzi wa kwanza Libya baada ya utawala wa kidikteta wa Gaddafi

17:44 - July 10, 2012
Habari ID: 2365439
Matokeo ya kura zilizokwisha hesabiwa za uchaguzi wa Bunge la Taifa la Libya yanaonesha kuwa kundi la wanaharakati wa Kiislamu linaloongozwa na Mustafa Abdul Jalil na chama kipya cha Muhammad Balhaj vinachuana vikali kwa ajili ya kupata viti vingi zaidi vya bunge.
Wakati huo huo Muungano wa Kitaifa unaoongozwa na Mahmoud Jibril unadai kuwa unaongoza kwa kuwa na viti vingi katika miji mikubwa kama Tripoli na Benghazi. Muungano huo unajumuisha pamoja vyama 40 vya siasa.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa baadhi ya nchi za Magharibi kama Ufaransa na Italia ambazo zinagombania hisa kubwa ya utajiri wa mafuta ya Libya zililiunga mkono kundi la Mahmoud Jibril katika uwanja wa siasa wa Libya. Jibril ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa serikali ya mpito ya Libya alijiuzulu nafasi hiyo baada ya wanamapinduzi kumtuhumu kwamba alikuwa na uhusiano na utawala wa zamani wa nchi hiyo.
Pamoja na hayo makundi ya Kiislamu pia yamepata nafasi nzuri katika uchaguzi wa Bunge la Taifa la Libya. Vyombo vya habari vya Magharibi vinamtaja Mustafa Abdul Jalil kuwa ni kiongozi wa tawi lenye misimamo ya wastani na Muhammad Balhaj kuwa ni kiongozi wa tawi lenye misimamo mikali. Kwa msingi huo nchi ya Libya inaweza kugawanywa katika maeneo matatu kwa kuzingatia mirengo ya kisiasa. Eneo la mashariki linalodhibitiwa na kundi lenye misimamo ya wastani, magharibi linadhibitiwa na maliberali watu wenye sera za Ulaya na Marekani na eneo la kusini lililo mikononi mwa makundi ya kikabila.
Uchaguzi wa tarehe 7 Julai ulikuwa wa kwanza kufanyika Libya baada ya kung'olewa madarakani utawala wa kidikteta wa Muammar Gaddafi uliodumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40. Wapigaji kura waliwajibika kuchagua wawakilishi wao 200 wa Bunge la Taifa. Tume ya Uchaguzi ya Libya imesema kuwa asilimia 60 ya watu waliotimiza masharti walishiriki katika zoezi hilo.
Bunge la Taifa au Majlisi ya Waasisi itakuwa na jumuku la kutunga sheria na mbali na kubuni katiba mpya ya Libya itakuwa pia na wajibu wa kuunda serikali mpya.
Bunge hilo litateuwa kamati ya kutunga katiba ambayo baadaye itapigiwa kura ya maoni na wananchi. Baraza la Mpito la Libya ambalo ndilo linaloendesha masuala ya Libya kwa sasa litavunjwa sambamba na kufanyika kikao cha kwanza cha Bunge la Taifa ambalo ndilo litakalochukua mamlaka yake.
Msemaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Libya amesema kuwa wananchi wote wa Libya ndio washindi halisi wa uchaguzi huo na wameweza kuiondoa madarakani serikali ya kidikteta iliyotawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 42.
1049573
captcha