IQNA

Sheria ya kuwaadhibu wanaovunjia heshima matukufu ya Kiislamu yapasishwa Tunisia

17:38 - July 18, 2012
Habari ID: 2372126
Chama cha Kiislamu cha al Nahdha nchini Tunisia kimetoa ripoti mwishoni mwa mkutano wake mkuu kikitangaza kuwa kimepasisha sheria ambayo kwa mujibu wake aina yoyote ya kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu na kufanya juhudi za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel vinahesabiwa kuwa ni kosa la jinai.
Taarifa ya chama cha al Nahdha imesisitiza juu ya udharura wa kupigwa marufuku hatua yoyote ya kujenga uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na kukabiliana na watu wanaovunjia heshima matukufu ya kidini.
Taarifa hiyo iliyosomwa na Waziri wa Afya wa Tunisia pia imesisitiza juu ya ulazima wa kuanzishwa serikali iliyostaarabika kwa msingi wa thamani za Kiislamu na matunda ya tajiriba ya mwanadamu.
Sehemu nyingine ya taarifa ya chama cha al Nahdha nchini Tunisia imesema kuwa maudhui ya Palestina itaendelea kuwa kadhia muhimu zaidi ya umma wa Kiislamu na kwamba juhudi za aina yoyote za kujaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Israel zinahesabiwa kuwa ni kosa la jinai.
Chama cha al Nadha pia kimetaja mfumo wa bunge wa Tunsia kuwa ndio mbinu bora zaidi ya kutimiza matakwa ya wananchi katika siku za usoni na imelitaka Baraza la Katiba kutilia maanani mapendekezo hayo.
Chama cha Kiislamu cha al Nahdha kilishinda uchaguzi wa kwanza wa Bunge uliofanyika mwaka huu nchini Tunisia baada ya kung'olewa utawala wa kidikteta wa Zainul Abidin Bin Ali. Dikteta huyo amekimbilia nchini Saudi Arabia ambako amepewa hifadhi na watawala wa kifalme wa nchi hiyo. 1056474

captcha