IQNA

Mashindano ya Qur'ani ya mwezi wa Ramadhani kufanyika New York

12:23 - July 30, 2012
Habari ID: 2380775
Kituo cha Mashia cha Ithna-Asheri mjini New York nchini Marekani kimepanga kuandaa mashindano ya hifdhi na kiraa ya Qur'ani Tukufu kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mashindano hayo ambayo yatafanyika tarehe 21 Ramadhani yatawajumuisha watoto wa kike na wavulana walio na umri wa chini ya miaka 18.
Katika kundi la hifdhi, washiriki watagawanywa katika makundi manne ambapo watatakiwa kuhifadhi sura za Masad kwa watoto walio na umri wa kati ya miaka 3 na 4, hifdhi ya aya mbili za mwisho za sura ya Baqarah kwa watoto walio na umri wa kati ya miaka 5 hadi 6, hifdhi ya sura ya A'la kwa watoto walio na umri wa kati ya miaka 7 hadi 8 na hifdhi ya sura ya Ghashia kwa watoto walio na umri wa kati ya miaka 9 hadi 11.
Kundi la kiraa litagawanywa sehemu mbili ambapo ya kwanza itawashirikisha washindani walio na umri wa kati ya miaka 11 hadi 14 na la pili la vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 18.
Mashindano hayo pia yatahusu hifdhi ya dua za Kiislamu kwa watoto walio na umri wa miaka 10 hadi 14. Mashindano hayo yatafanyika kwa lengo la kuwahamasisha vijana wa Kiislamu kujishughulisha zaidi na masuala ya Qur'ani Tukufu na hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Washindi wa kila kundi wataarifishwa na kuzawadiwa zawadi nono katika siku ya Idi. Kituo hicho cha Kiislamu pia kimekuwa kikitekeleza ratiba maalumu katika mwezi huu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuhitimishwa kiraa ya Qur'ani, warsha ya masomo ya Ramadhani, swala za jamaa, usomaji wa dua mbalimbali maalumu kwa mwezi huu ikiwa ni pamoja na dua za Jaushan Kabir na Mujir. Sherehe za idul Fitr pia zimo katika ratiba ya kituo hicho. 1065177
captcha