IQNA

Maqari wakongwe wa Qur’ani kutoka Nchi za ASEAN waenziwa huko Kuala Lumpur

17:47 - September 03, 2025
Habari ID: 3481180
IQNA – Maqari wakongwe wa Qur’ani kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) wamepongezwa kwa mafanikio yao katika Jukwaa la Kimataifa la Uhakiki wa Ijazah za Qur’ani na Kuheshimu Maqari wa ASEAN, lililofanyika nchini Malaysia.

Ijazah ya Qur’ani ni cheti kinachotolewa na mwalimu mwenye sifa stahiki kwa mwanafunzi, kuthibitisha kuwa ameihifadhi Qur’ani kwa kanuni sahihi na matamshi sahihi. Ijazah pia inaweza kutolewa kwa usomaji sahihi bila kuhifadhi.

Kila ijazah huorodhesha mlolongo wa walimu waliopitisha elimu hiyo kutoka kwa mwenye ijazah hadi kwa maimamu wa usomaji wa Qur’ani.

Katika jukwaa hilo, ambalo limehitimishwa jijini Kuala Lumpur, maqari waandamizi kutoka nchi wanachama wa ASEAN waliopata ijazah yenye mlolongo wa walimu waliothibitishwa, walienziwa kwa mchango wao katika kuhudumia na kufundisha Qur’ani Tukufu.

Maulamaa waandamizi pamoja na maelfu ya wahifadhi wa kiume na wa kike kutoka nchi za ASEAN walihudhuria tukio hilo.

Jukwaa hilo, lililoandaliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Waislamu (MWL), lililenga kuchunguza changamoto zinazohusiana na uhakiki wa ijazah za Qur’ani na kutoa mapendekezo ya suluhisho madhubuti.

Lengo lake lilikuwa kuzuia utoaji holela wa ijazah kwa wale wasio na ujuzi wa kutosha, ili kulinda ubora wa usomaji na ufundishaji wa Qur’ani Tukufu, kwa mujibu wa MWL.

Pia lililenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi maalum, kurahisisha ubadilishanaji wa maarifa, na kuunganisha juhudi za pamoja.

Katibu Mkuu wa MWL, Sheikh Mohammad bin Abdulkarim Al-Issa, ambaye aliongoza jukwaa hilo, alishuhudia kuenziwa maqari mashuhuri kutoka nchi za ASEAN, kwa mchango wao katika kueneza na kufundisha Kitabu Kitukufu, na kwa juhudi zao katika kulea vizazi vya wakariri wa Qur’ani.

Aidha, alishuhudia mahafali ya kundi jipya la wahifadhi wa kiume na wa kike waliopata ijazah ya Qur’ani kupitia Kituo cha Kimataifa cha Usomaji wa Kiufundi cha MWL.

Kundi la wanafunzi kutoka Taasisi ya Kuhifadhi na Kusoma Qur’ani ya Taasisi ya Kiislamu nchini Malaysia, inayohusiana na MWL, pia walihitimu katika jukwaa hilo.

3494444

Habari zinazohusiana
Kishikizo: qurani tukufu malaysia
captcha