Ayatullah Mohammad Hassan Akhtari, ambaye ni mkuu wa Makao Makuu ya Kumbukumbu ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu, ametoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Tehran, Jumatano.
“Leo hii, hata jamii zisizo za Kiislamu zinatoa msaada na kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina wanaoonewa. Lakini Ummah wa Kiislamu unapaswa kuchukua nafasi yake ipasavyo, na serikali pamoja na viongozi wa Kiislamu wanapaswa kuchukua hatua madhubuti,” alisema.
Kwa mujibu mwanazuoni huyo, moja ya malengo muhimu ya Wiki ya Umoja ni kutumia fursa ya kumbukumbu ya miaka 1500 tangu kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), ili kwa idhini ya Allah, dunia iweze kuelewa kwa undani dhulma wanayopitia watu wa Palestina.
“Tatizo la Palestina si jambo la kihistoria tu, bali ni tatizo la sasa linaloendelea kila siku. Kila siku tunashuhudia maelfu ya mashahidi na watoto wanaopoteza maisha. Njaa, umasikini, na ukosefu wa huduma za afya na maisha ni miongoni mwa maumivu makubwa yanayowakumba Wapalestina, hasa huko Gaza.”
Siku ya 17 ya Rabi al-Awwal, inayosadifiana na Septemba 10 mwaka huu, inaaminika na Waislamu Shia kama siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), wakati Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaamini kuwa siku ya 12 ya Rabi al-Awwal (Ijumaa, Septemba 5) ni siku ya kuzaliwa kwa Mtume wa Mwisho.
Ili kuziba hitillafu zilizopo kuhusu tarehe hiyo, kipindi kilichopo kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu na hayati mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, mwaka 1980.
Ayatullah Mohammad Hassan Akhtari amesema “Umoja wa Waislamu ni jambo la msingi sana, limehimizwa kwa mantiki ya kiakili, kibinadamu, na kwa misingi ya mafundisho ya dini, hasa katika Uislamu na kwa Mtume wetu mpendwa (SAW). Katika Qur’an Tukufu, Mwenyezi Mungu amesisitiza wazi umuhimu wa kuwa Ummah mmoja.”
Mkutano mkubwa wa kimataifa wa Wiki ya Umoja utafanyika chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu, ambapo inatarajiwa kuwa vituo vya utafiti na taasisi za kielimu zitatoa maudhui mapya na tafiti za kina kuhusu umuhimu wa umoja wa Ummah wa Kiislamu, mafundisho ya Ahlul-Bayt (AS), na maisha ya Mtume (SAW), na kazi hizo zitatafsiriwa kwa lugha mbalimbali na kusambazwa duniani.
Kwa mwaka huu, Wiki ya Umoja inaadhimishwa wakati ambapo Waislamu wa Gaza wanakabiliwa na mashambulizi ya kinyama kutoka kwa utawala wa Israel. Tangu Oktoba 7, 2023, zaidi ya Wapalestina 64,000—hasa wanawake na watoto—wameuawa, na wengi kujeruhiwa. Vifo vingi pia vimesababishwa na njaa kutokana na mzingiro wa Israel dhidi ya eneo la Gaza.
3494466