IQNA

Shahriari: Heshima ya Binadamu, Haki, na Usalama ni Nguzo Tatu za Umoja wa Kiislamu

11:04 - September 06, 2025
Habari ID: 3481190
IQNA – Akizungumzia heshima ya binadamu, haki, na usalama kama nguzo kuu tatu za umoja wa Kiislamu, mwanazuoni mwandamizi wa Kiirani amesema kuwa Palestina ni alama au nembo ya mshikamano wa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukaribisha Madhehebu ya Kiislamu (WFPIST), Hujjatul-Islam Hamid Shahriari, alizungumza kabla ya khutba ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran, na kusisitiza kuwa umoja wa Kiislamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa ni lazima uimarishwe ili kukabiliana na ubabe wa upande mmoja wa Marekani.

Aliwapongeza waumini kwa kuwadia kwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, akieleza kuwa WFPIST imekuwa ikihifadhi fikra hii ya thamani kwa miaka 38 kupitia Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, na imefikisha ujumbe wa mshikamano kwa ulimwengu mzima.

Mwaka huu, kwa kuadhimisha miaka 1500 tangu kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu Muhammad (SAW), Mkutano wa 39 wa Umoja wa Kiislamu wenye kaulimbiu "Mtume wa Rehema" utafanyika kuanzia Jumamosi hadi mwisho wa wiki.

Nguzo za Umoja wa Kiislamu

Katika kufafanua dhana ya umoja, Hujjatul-Islam Shahriari alieleza kuwa kuna angalau thamani tatu za Kiislamu zinazounda msingi wa mshikamano:

  1. Heshima ya Binadamu Mwenyezi Mungu amewatunuku wanadamu heshima ya kipekee: “Na kwa yakini tumewatukuza wanaadamu...” (Surah Al-Isra, aya ya 70) Heshima hii si ya Wairani tu, Waislamu au watu wa dini za mbinguni bali kila binadamu anastahili kuheshimiwa kwa sababu ya ubinadamu wake. Umoja wa jamii hujengwa juu ya heshima hii ya kiungu.
  2. Haki na Uadilifu Kila binadamu ana haki za msingi: haki ya kuishi bila kuuawa na madhalimu, haki ya kuishi kwa uhuru bila vizuizi, haki ya makazi, chakula, maji, na maisha yenye staha. Kuheshimu haki hizi ni msingi wa uadilifu wa kweli.
  3. Usalama Binadamu wote wana haki ya kuishi kwa amani iwe nyumbani, shuleni, msikitini, hospitalini au kazini. Mtu yeyote anayevuruga usalama huu ni adui wa mshikamano wa kibinadamu.

Palestina: Alama ya Mshikamano wa Dunia

Hujjatul-Islam Shahriari aliongeza kuwa Palestina imekuwa alama ya mshikamano kwa sababu nguzo hizi tatu yaani heshima, haki na usalama, zimekiukwa vibaya. "Hata wasiokuwa Waislamu wanaitetea Palestina kwa sababu wanatambua thamani ya utu, haki na usalama."

"Sifa hizi tatu—heshima ya binadamu, haki, na usalama—zinaeleweka kwa kila mwanadamu, na ndiyo maana hata wasiokuwa Waislamu wanaitetea Palestina. Kutetea heshima ya binadamu, haki, na usalama si jambo la Waislamu pekee; kwa hivyo, katika mitaa ya nchi za Magharibi, watu hujitokeza kwa wingi kuunga mkono Palestina na kulaani utawala wa Israel."

Ujumbe wa Qur’an na Wito kwa Waislamu

Aidha msomu hiyo alinukuu aya tukufu ya Qur'ani isemayo: “Shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msifarakane.” (Surah Al-Imran, aya ya 103) Akasema kuwa kila kitu kinachosababisha mgawanyiko ni haramu. Waislamu wa Sunni na Shia wanapaswa kusimama pamoja dhidi ya maadui kwa kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu.

Ushirikiano wa Kikanda

Kuhusu umuhimu wa umoja wa Kiislamu baina ya nchi za Kiisalmu katika eneo la Asia Magharibi, alisema: "Lazima tuzingatie kwa makini nchi jirani na zile za Kiislamu; nchi kama Pakistan, Uturuki, Saudi Arabia, na Misri ni muhimu sana. Tunapaswa kuimarisha hisia za udugu na nchi hizi. Hasa Misri, ambayo wakati mmoja iliungana na nchi 20 za Kiislamu kulaani shambulio la (utawala wa Israeli) dhidi ya Iran (mnamo Juni). Hizi ndizo uwezo wa ulimwengu wa Kiislamu, na taifa lililoungana lazima litegemee kamba ya Mwenyezi Mungu ili kuzuia uingiliaji wa adui."

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Wiki hii huadhimishwa kati ya tarehe 12 na 17 ya mwezi wa Rabi al-Awwal, tarehe ambazo Sunni na Shia huamini kuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW). Wiki hii ilitangazwa na Imam Khomeini katika miaka ya 1980 kama ishara ya kuleta umoja miongoni mwa Waislamu.

3494485

captcha