IQNA

Mafundisho ya Mtume (SAW) kwa lugha ya kisasa ni daraja zama za kale na zama hizi

15:43 - September 13, 2025
Habari ID: 3481223
IQNA – Mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), yakielezwa kwa lugha ya leo, yanaweza kusaidia kuziba pengo kati ya zama za kale na maisha ya kisasa, sambamba na kukabiliana na tatizo la ujinga wa kidini, kwa mujibu wa mwanazuoni mmoja kutoka Iran.

Hujjatul-Islam Ali Karami-Fereydouni, mtafiti wa masuala ya dini na mwandishi wa kitabu Utamaduni Kutoka kwa Mafundisho ya Muhammad (SAW), alisema kuwa ujumbe mwingi wa Mtume umebaki kuwa wa kudumu, lakini unahitaji uwasilishaji wa kisasa. Akizungumza na IQNA, alieleza nafasi ya mafundisho ya Mtume (SAW) katika jamii za leo.

“Mafundisho ya dini yamefungamana na maumbile ya mwanadamu, dhamira, akili, na jitihada za kutafuta elimu na uzuri. Thamani hizi hazipotei kamwe,” alisema. Hujjatul-Islam Karami-Fereydouni aliongeza kuwa misingi kama haki, uhuru, demokrasia, na uaminifu bado ni muhimu leo kama ilivyokuwa karne zilizopita.

Alifafanua kuwa baadhi ya dhana zinahitaji kufasiriwa upya kwa muktadha wa sasa. “Zamani watu walizungumza kuhusu ‘mashauriano.’ Leo, dhana hiyo imejidhihirisha kama ‘uchaguzi huru na wa haki.’ Wakati wengi wanapopiga kura, hakuna mwenye haki ya kubatilisha matokeo. Kufuata matakwa ya walio wengi ni wajibu wa kidini na kijamii,” alisema.

Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, baadhi ya masuala ya kidini ni ya kudumu, lakini mengine hubadilika kulingana na wakati na mahali, hivyo yanahitaji tafsiri mpya. “Mafundisho ya dini yanaweza kuendelea kuwa hai na yenye athari,” alisisitiza.

Akizungumzia nafasi ya maadili katika maisha ya Mtume, Karami-Fereydouni alirejea aya ya Qur’ani inayomtaja Mtume kama “Rehema kwa walimwengu wote” (Surat al-Anbiya, 21:107). Alinukuu kauli maarufu ya Mtume: “Nimetumwa kukamilisha tabia njema.” Alisisitiza kuwa maadili si adabu tu, bali ni pamoja na uaminifu, kuanzia kuhifadhi mali ndogo hadi kulinda hazina ya taifa.

Mwanazuoni huyo pia alitaja “ujinga wa kidini” kuwa changamoto kubwa ya kiutamaduni inayozikabili jamii za Kiislamu leo. “Misimamo mikali katika ulimwengu wa Kiislamu hutokana na tafsiri potofu, elimu duni, na kutokutekeleza yale yanayohubiriwa. Haya ni madhara ya kiutamaduni yanayoathiri dini,” alisema.

Alipoulizwa ni masuala gani Mtume (SAW) angeyapa kipaumbele lau angeishi leo, Karami-Fereydouni alitaja matatu: kuhimiza watu kuelewa ubinadamu na Muumba wao, heshima kwa haki za wengine, na kupambana na unafiki kati ya maneno na vitendo.

Alihitimisha kwa kusema kuwa Mtume (SAW) angewasilisha masuala haya kwa namna inayogusa nyoyo za watu wa leo. “Angewasilisha misingi ya kiulimwengu inayovuka mipaka na zama, misingi ambayo watu kote duniani bado wanaisaka,” alisema Karami-Fereydouni.

3494573

captcha