BRICS ni kifupi cha majina ya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini – nchi tano zilizoanzisha umoja huo kwa lengo la kukabiliana na utawala wa kibeberu wa Magharibi.
Mwaka jana BRICS ilipanuka na kujumuisha Iran, Misri, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu. BRICS sasa inawakilisha asilimia 45 ya watu duniani, asilimia 25 ya biashara ya kimataifa, asilimia 40 ya uzalishaji wa mafuta duniani na asilimia 28 ya Pato Ghafi la Taifa.
Mkutano wa viongozi wa kidini wa Kiislamu kutoka nchi wanachama wa BRICS ulifanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil, tarehe 4 Septemba 2025.
Iran iliwakilishwa na Hujjatul-Islam Mohammad Mehdi Imanipour, Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu.
Mwisho wa mkutano huo, washiriki walitoa tamko rasmi kuhusu msimamo wao juu ya masuala muhimu ya kimataifa. Tamko hilo lilisema:
Sisi, viongozi wa kidini wa nchi za Kiislamu wanachama wa BRICS, tukijikita katika misingi ya kiroho na kimaadili inayotufundisha kuheshimiana, kuwa ndugu, na kushirikiana katika mema na uchamungu; tukivutiwa na mafundisho ya Uislamu yaliyomo ndani ya turathi tajiri za fiqh ya Kiislamu; tukitambua wajibu wetu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na vizazi vijavyo kama viongozi wa kidini wa kuhifadhi na kuimarisha misingi ya maadili ya jamii inayodhamini ustawi wa watu na mataifa; na tukizingatia kuwa kipengele cha kiroho cha watu wetu ni miongoni mwa nguzo muhimu za kuleta ukaribu ndani ya umoja huu wenye utofauti mkubwa – kwa kauli moja tunathibitisha yafuatayo:
Kanuni ya umoja katika utofauti imejikita kwa kina katika mafundisho ya Uislamu, ambayo yanaeleza kuwa hekima ya Mwenyezi Mungu katika tofauti za kibinadamu na kikabila ni ishara ya utukufu Wake. Kanuni hii inaakisi azma yetu ya pamoja ya kujenga dunia yenye mfumo wa pande nyingi, isiyolazimisha mfumo mmoja, bali inayojengwa juu ya kuheshimu mila za kale, tamaduni, dini na sifa za ustaarabu.
Tunaunga mkono kwa dhati sera za viongozi na serikali za nchi zetu ndani ya mfumo wa BRICS, pamoja na juhudi zao zisizokoma za kulinda na kukuza maadili ya kiroho na kimaadili ambayo ustaarabu wa binadamu umejengwa juu yake kwa karne nyingi. Tunakataa kwa nguvu zote utawala wa itikadi zinazopingana na maumbile ya mwanadamu.
Kwa kuzingatia utofauti wa kitamaduni uliojaa utajiri miongoni mwa watu wa nchi wanachama, kuimarisha na kuendeleza mazungumzo ya kidini na kikabila ni kipengele muhimu cha kuendeleza ushirikiano wa kujenga na wenye tija ndani ya umoja huu.
Tunaamini kuwa kuvunjika kwa muundo wa familia yenye afya ni tishio kubwa kwa mustakabali wa ubinadamu. Kutokana na hali ya sasa, jukumu letu la msingi na la haraka ni kufanya kila juhudi kuhifadhi na kukuza maadili bora ya familia miongoni mwa vijana, ikiwemo kwa kushirikiana kwa karibu na wawakilishi wa dini nyingine na nguvu zote zenye afya ndani ya jamii.
Tukitambua uwezo mkubwa wa akili bandia (AI) katika maendeleo ya nyanja nyingi za maisha ya binadamu na katika kutatua matatizo ya dunia, tunatoa wito wa matumizi ya AI na udhibiti wa viwango vyake kufuata misingi ya maadili.
Tunalaani kwa uwazi na kwa nguvu zote aina zote za uchochezi wa chuki, misimamo mikali, ugaidi na ufashisti. Pia tunatangaza kuwa dharau yoyote dhidi ya dini, pamoja na mwelekeo wowote wa kuzuia haki na uhuru wa waumini, haikubaliki.
Tunatoa wito wa kuimarisha maslahi yetu ya pamoja katika kupanua ushirikiano wa kisayansi, kidini na kibinadamu kati ya jamii na mashirika ya Kiislamu katika nchi zetu.Kwa msingi huo, washiriki wa mkutano huu wanatoa shukrani za dhati kwa waandaaji wa tukio hili muhimu na la kipekee, na kwa msaada wao kamili katika kulitekeleza.
Tunathamini juhudi maalum za serikali, jamii na viongozi wa kidini wa Brazil, kwa msingi wa utu na usawa, katika kukuza uelewano baina ya watu na tamaduni, kuunganisha ustaarabu, kushirikiana baina ya nchi na mabara, na kudumisha ustawi na mafanikio ya mataifa na jamii.
3494474