Hujjatul Islam Seyed Mostafa Hosseini Neyshabouri, mkurugenzi mkuu wa Idara ya Tabligh (uenezaji) katika Shirika la Iran la Utamaduni na Uhusiano wa Kiislamu (ICRO), amebainisha mchakato wa kuunda bunge la Qur'ani la ulimwengu wa Kiislamu katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA).
Hapa chini ni sehemu ya mazungumzo yake: Kwa muda mrefu, fikra za wale wanaojishughulisha na diplomasia ya Qur'ani zimekuwa zikishughulika na muktadha na mifumo ambayo Qur'ani inaweza kuanzisha mitandao ya kuleta umoja na mshikamano ili ulimwengu wa Kiislamu utatue matatizo yake kwa kutumia Qur'ani. Fikra hii ilikuwepo kwa muda mrefu hadi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia mkuu wa ICRO, ilipowasilisha wazo hili katika kikao cha 20 cha Jukwaa la Kimataifa ya Waislamu, kilichofanyika Moscow mwaka jana kwa ushiriki wa nchi 41. Lengo ni kuunda mtandao ndani ya fremu ya Bunge la Qur'ani la Ulimwengu wa Kiislamu ili tuweze kutatua matatizo ya Waislamu kwa kutumia misingi ya Qur'ani. Ni vizuri kuwa na shughuli katika uwanja wa Qur'ani, lakini si kamili na haziwezi kutatua matatizo katika maeneo mbalimbali ya maisha au katika maeneo ya elimu, maisha ya kijamii, na roho, basi hazijafikia malengo yake ya juu.
Pia, mojawapo ya matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu ni kwamba maadui wanajitahidi kutuvuruga na kuharibu nguvu zetu na uwezo wetu kwa kutumia mgawanyiko na nukta zinazoibua hitilafu. Lakini tunaweza kuyazuia haya kwa kutumia mafundisho ya kina ya Qur'ani Tukufu na kutumia uwezo wake mkubwa. Ikiwa ulimwengu wa Kiislamu ungekuwa na umoja na upendo, matatizo yote wanayokutana nayo Waislamu leo yangeweza kutatuliwa, na masuala kama Gaza, Palestina na Syria hayangejitokeza kabisa. Tunayo mhimili bora, ambao ni muujiza, na sote tunaweza kuhisi muujiza huo sasa hivi, na dhana zake za ufunuo zinaweza kutumika katika nyanja mbalimbali baada ya kuzifasiri na kutafsiri. Naamini kuwa hii ni suluhisho kwa matatizo yote ya ulimwengu wa Kiislamu na kwa kweli, ulimwengu wa ubinadamu. Kuhusu maandalizi ya kuanzisha Bunge la Qur'ani la Ulimwengu wa Kiislamu, tulikuwa na mikutano ya kina sana.
Baada ya mjadala huu, wazo hili lililetwa kwa umakini katika majadiliano mbalimbali na mikutano na wasomi na wazee wa ulimwengu wa Kiislamu, na kila mtu alikubali au alikiri kuwa kuna haja ya kuwa na shirika la Qur'ani kama hili. Kuhusu wazo kuu na pia muundo na kanuni zinazopendekezwa, tulikuwa na mikutano mizuri na wataalamu na wanaharakati wa uwanja huu. Tulikutana na rais mpendwa wa shirika la JAKIM, ambalo ni taasisi muhimu ya kidini nchini Malaysia, pamoja na viongozi wakuu wa Qur'ani na kidini kutoka Indonesia. Tulisafiri kwenda Iraq na kufanya mikutano na idara za Waqf za Shia na Sunni, pamoja na vituo vya Dar al-Quran na viongozi mashuhuri wa semina za Kiislamu.
Tulifanya kikao cha awali cha Bunge la Qur'ani la Ulimwengu wa Kiislamu na wasomi wa Qur'ani kutoka Lebanon, Bosnia na Herzegovina, na nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Mufti Mkuu wa Uganda. Katika mkutano huo, kikao cha awali kilipangwa ili kuelewa vyema wazo hili na utekelezaji wake, na zaidi ya nchi 20 zilihudhuria. Tuliafikiana kuwa, baada ya kupata maoni, tunaweza kufikia makubaliano na kuelewana katika ulimwengu wa Kiislamu na miongoni mwa wasomi na wanazuoni wa Qur'ani. Rasimu ya kanuni, baada ya kuidhinishwa katika duru za ndani na kisha katika duru za ulimwengu wa Kiislamu na muhimu zaidi, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, inapaswa kupitishwa, na baada ya hapo, mchakato wa kuanzisha sekretarieti yake kwa ajili ya uanachama wa wanachama wakuu na wanachama wa kamati utaundwa.
Huu ni mchakato ambao utachukua muda, lakini unaendelea mbele. Kumekuwepo na maendeleo mazuri, ikizingatiwa kuwa hakuna shaka kuhusu umuhimu wa kuunda bunge hili. Tumevuka hatua ya kujadili umuhimu wake na sasa tupo katika mchakato wa kuunda, na kwa bahati nzuri, makubaliano yaliyopo yanawezesha kazi kuendelea kwa kasi zaidi. Kulingana na ratiba yetu, kanuni za Bunge la Qur'ani la Ulimwengu wa Kiislamu zitakamilika mwishoni mwa Septemba na kuwasilishwa kwa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu. Ingawa mikutano kadhaa ya awali imefanyika, mikutano mingine ya awali inapangwa, kisha sekretarieti yake itaaanza rasmi kazi wakati kanuni zitakapothibitishwa na OIC.
4302356