IQNA

Mtazamo

Mtaalamu: Shambulizi la Israeli dhidi ya Qatar limethibitisha usahihi wa sera za Iran

13:13 - September 14, 2025
Habari ID: 3481228
IQNA – Shambulizi la hivi karibuni la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Qatar limethibitisha usahihi wa sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kipindi cha miaka 45 iliyopita, hususan kuhusu msimamo wa kutokufanya maridhiano na utawala wa Tel Aviv. Hayo ni kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya Asia ya Magharibi.

“Kwa sasa, mwelekeo wa kuungana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeenea katika nchi nyingi za Kiarabu, na hili ni fursa adhimu kwetu,” alisema Jaafar Qanadbashi katika mahojiano na Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA).

Utawala wa Israel ulitekeleza shambulizi la anga dhidi ya Doha Jumanne iliyopita kwa lengo la kuwaua wajumbe wa kisiasa wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas.

“Huenda ujumbe wake muhimu zaidi, ambao haujapewa uzito katika vyombo vya habari, ni hofu kubwa ya Wazayuni kuhusu kuundwa kwa taifa huru la Palestina.”

Akizungumzia lengo la Wazayuni la kuwaua kigaidi au kuwadhoofisha viongozi wa kisiasa wa Palestina, alisema kuwa wanajaribu kuunda ombwe la uongozi kwa kuwaondoa maafisa na watu mashuhuri wanaoweza kuongoza serikali ya Palestina, ili hatimaye asiwepo mtu mwenye sifa za kuiongoza.

Qanadbashi aliongeza kuwa hofu hii inatokana na mwelekeo wa sasa katika Umoja wa Mataifa na ngazi ya kimataifa unaoashiria kuongezeka kwa uungwaji mkono wa kutambuliwa kwa taifa la Palestina.

Mtaalamu huyo alibainisha kuwa katika Umoja wa Mataifa, aghlabu ya nchi zimetangaza rasmi kutambua taifa la Palestina, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na matamanio ya utawala wa Kizayuni ya kulifuta taifa hilo na kuzuia kuundwa kwake.

Aliuelezea mchakato huu kama “azma ya mataifa na serikali za dunia,” na akaongeza: “Katika ngazi ya wananchi, tunashuhudia harakati ya msafara mkubwa zaidi wa meli za misaada zikielekea Gaza, msafara unaojulikana kama Sumud na kusema hii ni ishara ya namna waliowengi duniani wanavyounga mkono Hamas na wananchi wa Palestina ili kuvunja mzingiro wa Gaza. Msafara wa kimataifa wa Sumud unajumuisha meli kadhaa zinazowakilisha mataifa mbalimbali, zikiwa na misaada ya kibinadamu.”

Akirejelea historia ya Wazayuni kuwashambulia viongozi wa Hamas, Qanadbashi alisema kuwa lengo lao ni kudhoofisha mstari wa kisiasa wa Hamas kwa kuwaondoa viongozi wake mashuhuri.

Shambulizi dhidi ya Qatar lililenga kuwaua viongozi wa mwisho wa Hamas. “Walimwua shahidi Ismail Haniyeh, Yahya Sinwar, na Muhammad Deif, hivyo sera yao ni kuunda ombwe la uongozi ndani ya Hamas. Ni wazi sera hii si sahihi.”

Alitathmini historia ya mashambulizi dhidi ya uongozi wa Hamas na kusema kuwa Hamas imepoteza viongozi wake kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita lakini imekuwa ikiwachagua warithi mara moja. “Tangu mwanzo, Sheikh Ahmed Yassin aliuawa shahidi, na chini ya mwezi mmoja baadaye, Abdel Aziz Rantisi naye aliuawa. Makamanda wengi waliuawa lakini warithi wao walichaguliwa mara moja.”

Akijibu swali kuhusu iwapo shambulizi la Israeli dhidi ya Doha linaendana na mpango wa “Israeli Kubwa,” alisema kuwa baadhi ya wachambuzi wanaona shambulizi hilo kama sehemu ya utekelezaji wa mpango huo, lakini mtazamo huo si sahihi. Tatizo la kwanza ni dhana ya kwamba Wazayuni wana nguvu kubwa, na pili ni kwamba Qatar si sehemu ya mpango wa Israeli Kubwa.”

Ramani ambayo Wazayuni wamekuwa wakipendekeza kwa miaka 70 inajumuisha maeneo kutoka Mto Nile nchini Misri hadi Mto wa Furat nchini Iraq, pamoja na sehemu za Jordan, Syria na Lebanon, alibainisha.

“Utawala wa Kizayuni hauko katika nafasi ya kujionyesha kuwa na nguvu, ingawa baadhi ya wachambuzi wanaounga mkono Wazayuni wanajitahidi kuonyesha hadharani kuwa Israel ina nguvu na kwamba itatawala Asia ya Magharibi. Lakini hali halisi si hivyo, na kupitiliza katika maelezo ya sasa si sahihi.”

Qanadbashi alisisitiza kuwa Israel ni utawala wa uvamizi, lakini ukweli ni kwamba haina uwezo wa kutekeleza mpango huo.

“Katika wiki mbili zilizopita, Wazayuni wamevamia zaidi ya nchi saba au nane za Kiarabu; walishambulia Tunisia kwa sababu ya meli zilizobeba misaada ya kibinadamu, pia walishambulia Syria, Lebanon, Yemen, na hata Palestina yenyewe. Mashambulizi haya yote yanatokana na hofu ya utawala wa Kizayuni, kwa sababu wanaogopa kuundwa kwa taifa la Palestina na uwezo wa mataifa ya eneo hili kumaliza uvamizi.”

Alisisitiza haja ya hatua za pamoja na za vitendo kutoka kwa nchi za Kiislamu dhidi ya vitendo vya utawala wa Kizayuni, akirejelea kauli ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao chake cha hivi karibuni na Rais na Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa nchi za Kiislamu kukatisha mahusiano ya kibiashara na kisiasa na utawala wa Israeli.

“Polepole, nchi nyingi za Kiarabu zimegundua kuwa njia ya maridhiano, makubaliano ya Abraham, na uhalalishaji wa mahusiano na Israeli ilikuwa kosa kubwa, kwa sababu Israeli haijaheshimu nchi hizo na imekuwa ikivamia maeneo yao mara kwa mara bila kuratibu nao. Kitendo cha kuwashambulia bila kuratibu ni dharau kwa nchi hizo.”

Kishikizo: qatar israel iran
captcha