IQNA

Mpango wa Mahufadh milioni 10 wa Qur’ani Iran wapongezwa

16:11 - July 30, 2012
Habari ID: 2381001
Mwanazuoni mmoja wa Misri ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mpango wake wa kuhakikisha kuna watu milioni 10 waliohifadhi Qur’ani nzima nchini.
Akizungumza wakati alipotembelea ofisi za IQNA mjini Tehran, Sheikh Tajuddin Hamed Abdullah al Hilali ambaye ni mkuu wa Ujumbe wa Qur’ani wa Misri nchini Iran amesema mpango huo wa Iran wa kutoa mafunzo kwa mahufadh na maqarii wa Qur’ani Tukufu ni ishara ya iradi na ustawi wa Iran katika masuala Qur’ani.
Ameashiria aya ya 9 ya Sura Isra isemayo: Hakika hii Qur'ani inaongoa kwenye yaliyo nyooka kabisa…" na kuongeza kuwa Qur’ani Tukufu ni Habl-ul-Matin (kamba yenye nguvu ya Allah), njia iliyonyooka na mhimili mkuu wa umoja wa umma wa Waislamu.
Sheikh Al Hilali aliyewahi kuwa Mufti wa Australia amesema, ‘Tunaamini kuwa kujifunza Qur’ani ndio njia bora ya kufikia umoja wa Waislamu na kukurubisha nyoyo za Waislamu.’
Sheikh Al Hilali pia ameashiria miongozo ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini RA kuhusu ustawishaji wa harakati za Qur’ani na kusema, ‘nilipokuja Iran kwa mara ya kwanza mwaka 1982, katika mkutano wangu na Imam Khomeini huko Jamaran, alisisitiza kuwa Iran inajitahidi kuwa kituo cha mahufadh wa Qur’ani Tukufu. Sasa katika safari hii, nilimsikia Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akizungumza kuhusu mpango wa kuwalea mahufadh milioni 10 wa Qur’ani nchini Iran. Hii ni ishara kuwa Iran imepiga hatua ili kuongoza katika suala la kuhifadhi Qur’ani.’
Mufti huyo wa zamani wa Australia amesisitiza kuwa wanazuoni wa Kishia na Kisuni katika vyuo vya kidini vya Qum, Iran na Al Azhar Misri wanapaswa kutekeleza miongozo ya Imam Khomeini RA kuhusu kudumisha umoja wa Kiislamu na kukabiliana na njama za maadui.
1064302
captcha