IQNA

Nakala za rangi za Qur'ani zazusha mjadala Saudia

16:11 - July 30, 2012
Habari ID: 2381083
Uchapishaji wa nakala za Qur'ani zenye rangirangi nchini Saudi Arabia umezusha misimamo tofauti kati ya waungaji mkono na wapinzani wa hatua hiyo.
Gazeti la kimataifa la al Sharq al Ausat limeripoti kuwa waungaji mkono wa kuchapishwa nakala za Qur'ani kwenye karatasi zenye rangi mbalimbali kunawavutia watoto kusoma kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu huku wapinzani wakisema kuwa suala hilo linashusha chini haiba na heshima ya Qur'ani.
Mhadhiri wa sheria za Kiislamu nchini Saudia Ibtisam al Muhammadi ambaye anapinga hatua hiyo anasema kuwa, uchapishaji wa Qur'ani katika karatasi zenye rangirangi unakishabihisha kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na vitabu vya visa vya watoto wadogo. Anasema ameshuhudia nakala ya aina hiyo ya Qur'ani na kwamba awali alidhani kuwa Qur'ani hiyo iliyoandikwa kwenye karatasi zenye rangi za njano, kijani na nyekundu ni daftari la kuchorea.
Al Muhammadi amevitaka vyombo husika nchini Saudi Arabia kuacha kusambaza nakala za aina hiyo za Qur'ani Tukufu.
Katika upande mwingine Muhammad al Saidi ambaye ni mkuu wa kitengo cha utafiti wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Ummul Quraa mjini Makka anasema uchapishaji wa nakala za Qur'ani katika karatasi zenye rangirangi unajuzu iwapo itafanyika kwa nia ya kuhudimia Qur'ani Tukufu. 1065988

captcha